MAAFISA sita wa polisi waliokamatwa kwa mauaji ya ndugu wawili katika Kaunti ya Embu watakaa rumande kwa siku 14 uchunguzi unapoendelea.
Hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Nairobi Bw David Ndungi alitupilia mbali ombi la washukiwa hao la kuachiliwa kwa dhamana akisema “haki zao binafsi haziwezi linganishwa na maslaha ya umma.”
Bw Ndungi alisema mauaji ya ndugu hao wawili Benson Njiru Ndwiga na Emmanuel Matura Ndwiga Agosti 1 2021 yalizua hisia kali kote nchini huku miito ikitolewa hatua kali zichukuliwe dhidi ya waliohusika.
“Kuwaachilia Koplo Benson Mbuthia , Koplo Consolata Kariuki , Konstebo Nicholas Sang Cheruiyot, Konstebo Martin Msamali Wanyama, Konstebo Lilian Cherono Chemuna na Konstebo James Mwaniki kwa dhamana ni kuhatarisha maisha yao,” alisema Bw Ndungi.
Hakimu huyo alisema mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji amewasilisha ushahidi kwamba washukiwa hao watavuruga mashahidi.
Maafisa sita wa polisi waliohusishwa na mauaji ya ndugu wawili kaunti ya Embu wafikishwa kortini.. Picha (2) Nelson Havi (kulia) aliwakilisha familia ya watoto hao pamoja na chama cha wanasheria nchini (LSK)…Picha/RICHARD MUNGUTI
DPP alieleza mahakama kupitia kwa viongozi wa mashtaka Tabitha Ouywa na Jacinta Nyamosi kwamba “hali katika eneo la Kianjakoma ni mbaya na endapo maafisa hao wa polisi wataachiliwa basi usalama utavurugwa.”
Bi Ouywa alisema ndugu hao walikufa katika mazingira ya kusikitisha sana.Alisema afisa wa mamlaka ya uchunguzi wa utenda kazi ya polisi IPOA kupitia kwa afisa anayechunguza kesi hiyo Bw Ibrahim Sunu anahitaji kupewa muda wa kutosha kuchunguza kesi hiyo.
Bw Ndungi alikubaliana na DPP pamoja na Rais wa chama cha wanasheria nchini LSK Nelson Havi waliosema washukiwa hao sita hawapasi kuachiliwa kwa vile watavuruga mashahidi.
Hakimu alisema washukiwa hao watavuruga ushahidi kwa vile wanajua watashtakiwa kwa mauaji ya ndugu hao wawili.Akipinga kuachiliwa kwa maafisa hao sita wa polisi , Bw Havi alisema gari walimokuwa wameigizwa ndugu hao iliteketezwa na polisi ili kuharibu ushahidi.
Bw Havi alisema maafisa wakuu katika idara ya Polisi waliwahamisha maafisa wakuu katika kituo cha Polisi cha Manyatta ambapo sita hao walikuwa wakihudumu.
“Mheshimiwa ushahidi muhimu ulitetekezwa moto na maafisa wa polisi waliotaka haki isitendeke,”alisema Bw Havi.
Aliendelea kueleza mahakama kuwa maafisa hao sita wa polisi walikuwa wamehamishwa vile vile lakini “miito ilitolewa na viongozi mbali mbali akiwamo Spika wa Bunge la Kitaida Justice Muturi ambaye pia ni wakili hatua madhubuti ichukuliwe dhidi ya maafisa hao wa polisi.”
Bw Havi alisema Benson alikuwa anasomea shahada ya Uhandisi ilhali Emmanuel alikuwa anasomea shahada ya Sheria.
Ndugu hao waliuawa kwa madai walikataa kufuata sheria za kafiu.Wote wawili waliuawa mnamo Agosti 1,2021.Maafisa hao watazuiliwa katika kituo cha Polisi cha Capital Hill hadi Agosti 31, 2021 watakaposhtakiwa kwa mauaji.
Na wakati huo huo Bw Havi aliomba sheria za kafyu zifutiliwe mbali akisema imeleta maafa.“Rais Uhuru Kenyatta na Serikali anapasa kuhakikisha chanjo za Corona zimetolewa kwa wananchi wote.Corona haisambazwi na giza. Kama hakungekuwa na kafyu Benson na Emmanuel hawangeuawa,”alisema Bw Havi.
Aliikashfu Bunge kwa kukataa kusimamia sheria kwa njia ipasayo na kuruhusu wananchi wanyanyaswe na afisi mbali mbali za kitaifa