Connect with us

General News

Hasara tele wanabiashara wakitorokea eneo salama kutokana na machafuko – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Hasara tele wanabiashara wakitorokea eneo salama kutokana na machafuko – Taifa Leo

Hasara tele wanabiashara wakitorokea eneo salama kutokana na machafuko

Na BARNABAS BII

WAFANYABIASHARA katika kaunti zinazokumbwa na ukosefu wa usalama eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, wanaendelea kupata hasara baada ya kufunga biashara zao wakihofia mashambulizi ya kulipiza kisasi licha ya ahadi za serikali kwamba imekomesha mizozo iliyosababisha vifo vya watu kadhaa na mamia kutoroka makwao.

Wafanyabiashara kadhaa katika kaunti za Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet na Baringo wamefunga biashara zao na kutoroka eneo hilo kufuatia mashambulizi mapya ambayo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 10 katika kipindi cha wiki mbili zilizopita licha ya serikali kuahidi kukabiliana vikalo na wahalifu wanaoyatekeleza.

Baadhi ya biashara zilizobaki zimefunguliwa hazipati bidhaa za kutosha jambo ambalo limeathiri mapato huku mashambulizi ya kulipiza kisasi ya majangili na mizozo ya mipaka yakivuruga maisha ya kijamii na uchumi ya wakazi.

Soko la Chesogon linalotumiwa na wafanyabiashara kutoka kaunti hizo tatu limethiriwa pakubwa na ukosefu wa usalama na kulazimisha baadhi ya wafanyabiashara kufunga kazi zao na kuhamia maeneo salama.

“Kushukiana kunaendelea miongoni mwa jamii zinazopingana ambako kumetia hofu wateja wetu. Hii imelazimisha baadhi ya wafanyabiashara kupunguza shughuli zao kwa hofu ya mashambulizi,” alisema Jackson Meriong’or, mfanyabiashara katika kituo cha Chesogon.

Soko hilo linalopatikana kwenye mpaka wa kaunti za Elgeyo-Marakwet na Pokot Magharibi lilikubwa na athari za maporomoko ya ardhi yaliyoua watu 23 miaka miwili iliyopita.

Eneo hilo linaendelea kukumbwa na mashambulizi ya kulipizana kisasi miongoni mwa wahalifu waliopata silaha kali kukabili maafisa wa usalama waliotumwa kutuliza hali.

Mashambulizi hayo mapya yamevuruga kufunguliwa kwa shule baada ya familia nyingi kuhamia maeneo salama.

Shule zilizoathiriwa zaidi ni zilizo karibu na kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet na kaunti ndogo za Baringo Kusini na Baringo Kaskazini ambako maelfu ya familia zimetoroka makwao kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara ya wizi wa mifugo na mizozo ya mpaka.

“Shule nyingi huenda zikose kufunguliwa kutokana na hali ya usalama. Tunataka usalama kuimarishwa katika taasisi za masomo,” alisema mbunge wa Sigor Peter Lochakapong.

Zaidi ya shule 20 za msingi na za sekondari zilizokuwa zimefungwa kutokana na tatizo la ukosefu wa usalama katika eneo hilo linalokubwa na visa vya ujangili zinatarajiwa kufunguliwa, kwa hisani ya misafara ya amani inayojumuisha viongozi wa kaunti za Baringo, Pokot Magharibi, Turkana na Samburu.

Sekta ya elimu iliathiriwa eneo hilo shule zikikosa kufunguliwa kwa sababu ya ukosefu wa usalama huku baadhi zikihitaji kujengwa upya baada ya kuharibiwa na majangili wanaojihami kwa silaha.

Maafisa wa utawala na usalama katika eneo hilo wanakiri kwamba wahalifu wanaotekeleza mashambulizi hayo bado hawajakamatwa, ishara ya uwezekano wanapanga mashambulizi zaidi.