Kingi amezewa ODM ikimkwaza
VALENTINE OBARA NA MAUREEN ONGALA
CHAMA cha Pamoja African Alliance (PAA) kinachoongozwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, huenda kikapata washirika wapya wa kisiasa wakati ambapo kuna misukosuko kati yake na chama cha ODM Pwani.
Mikwaruzano kati ya PAA na ODM ilidhihirika wazi wikendi, wakati wa maandalizi ya kampeni za urais za Bw Raila Odinga katika Kaunti ya Kilifi.
Ijapokuwa Bw Kingi alisisitiza kuwa bado ana nia ya kumpigia debe Bw Odinga kwa urais, imesemekana kuna mazungumzo yanayoendelea kati ya PAA na chama cha Wiper kinachoongozwa na Bw Kalonzo Musyoka kuhusu ushirikiano.
Akizungumza Jumapili akiwa katika ziara ya kisiasa Mombasa, Bw Musyoka alifichua kuwa mashauriano hayo yanalenga kusaidia muungano wake wa One Kenya Alliance (OKA) kupata nguvu zaidi katika maeneo ya Pwani kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
“Nia yetu ni kufagia viti vingi zaidi si Mombasa tu bali pia Kwale na Kilifi ikiwezekana, na tutakuwa pamoja na washirika wetu katika mpango kama huu. Tunajaribu kuzungumza na wenzetu kama vile PAA,” akasema Bw Musyoka.
Juhudi zetu za kutafuta maoni ya PAA kuhusu suala hilo ziligonga mwamba, kwani msemaji wa chama hicho, Bw Lucas Maitha, hakuwa amezijibu kufikia wakati wa gazeti la Taifa Leo kuchapishwa.
Katika mahojiano ya awali, Bw Maitha alithibitisha kuwa walimpa Bw Odinga nakala ya matakwa yao ikiwa watashirikiana katika muungano lakini bado hawajajibiwa.
“Kwa sasa hatuna makubaliano yoyote rasmi na Raila. Hatutaki hali ambapo mambo yanaharakishwa, kisha hati zinatiwa sahihi kwa pupa,” akasema Bw Maitha.
Mwaka uliopita, Bw Kingi aliibua gumzo alipokutana na vinara wa Muungano wa OKA, wakiongozwa na Bw Musyoka mjini Mombasa.
Gavana huyo aliyeasi ODM miaka michache iliyopita alijitokeza baadaye mwaka huu kutangaza kuwa atamuunga mkono Bw Odinga ila kupitia kwa chama chake kipya.
Wiki iliyopita, mizozano ya wanasiasa wa ODM na PAA ambayo imekuwa ikiendelea kwa muda sasa hasa katika Kaunti ya Kilifi, ilidhihirika wazi ODM iliposisitiza kuwa wenzao wa PAA hawakufaa kuhudhuria mikutano ya hadhara iliyoongozwa na Bw Odinga.
Hii ni licha ya kuwa, Bw Kingi kwa niaba ya chama hicho alichounda, alikuwa ametangaza awali kwamba wanaunga mkono azimio la Bw Odinga kwa urais.
Ilibainika kuwa wanachama wa ODM wanahofia huenda wenzao wa PAA wakatumia umaarufu wa Bw Odinga kushindania viti vya kisiasa dhidi yao, huku duru nyingine zikidai kuwa PAA iliwasilisha masharti magumu kwa Bw Odinga kuhusu ushirikiano katika muungano wa kisiasa.