Jinsi pingamizi za wandani wa Rais zilivyowapa wanabodaboda afueni
NA MWANGI MUIRURI
IMEIBUKA kuwa wandani wa Rais Uhuru Kenyatta wenye uelewa wa masuala ya siasa na uchumi ndio waliwapa wahudumu wa bodaboda afueni ya kusitishwa kwa msako mkali uliokuwa umezinduliwa dhidi yao.
Msako huo ulitokana na kisa ambapo wahuni waliojumuika pamoja na wachache wa bodaboda walimdhulumu mwanadiplomasia wa kike katika barabara ya Forest Road, Nairobi.
Duru zinasema kuwa msimu huu wa siasa kali za urithi wa Ikulu ulichangia pakubwa kubatilishwa kwa msako huo ilipoibuka kwamba vijana wengi walio katika sekta ya bodaboda walianza kutetewa na mirengo ya kisiasa.
“Wakati wa kusaka kura huwa na changamoto zake kwa kuwa ndio wakati ambapo sera na sheria hupindwa ili kufurahisha na kushawishi ufuasi. Kwa hili la bodaboda, hatukuwa na jingine ila tu kufutilia mbali ili kwanza tutafute kura,” akasema mbunge wa Kieni Bw Kanini Kega.
Vitengo vya kiusalama vilisema kwamba msako huo utarejelewa katika siku za baadaye baada ya jopokazi lililoundwa na Wizara ya Usalama na Maswala ya Ndani kuandaa ripoti.
Mwandani wa Rais Kenyatta kutoka Kaunti ya Murang’a Bw Peter Kenneth na anayesemwa kuwa atateuliwa kuwa Naibu wa Rais katika Ikulu ya Raila Odinga endapo mrengo wa Azimio La Umoja utafaulu kutwaa mamlaka alisema kwamba “msako huo ulikuwa sumu ya kisiasa kwa kuwa vijana kote nchini walikuwa wameanza kuchochewa kwamba serikali ilikuwa ikiwalenga kwa msingi wa ubaguzi wa hadhi ya kiuchumi.”
“Tulikuwa tumeanza kupigwa kisiasa tukisemwa kwamba sisi ni wafuasi wa serikali inayoenzi matajiri na kudhihaki maskini. Wahudumu walikuwa wameanza kujipanga katika maandamano huku nao polisi wakiwakabili kupitia fujo. Mazingira hayo hayakuwa na manufaa kiuchumi na kisiasa,” akasema Bw Kenneth.
Alisema kuwa msako huo ulikuwa umeanza kupindwa kisiasa ili kumtenga Rais na mrengo wake wa Azimio La Umoja kiasi kwamba Bw Odinga anayeungwa mkono kuwania urais katika mrengo huo alijitenga nao.
Bw Odinga alikinziana na amri ya rais akisema kwamba ulikuwa umezinduliwa na kutekeleza kwa njia isiyowiana na haki.
Jumamosi, aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Spoti Bw Zack Kinuthia alisema kwamba bodaboda huwa chini ya utaratibu wa trafiki siku zote na maafisa wa polisi hawafai kukumbushwa kutekeleza sheria.
Bw Kinuthia ambaye anawania kiti cha ubunge cha Kigumo kwa mrengo wa Azimio La Umoja alisema kwamba msako huo hauna mashiko ya uwazi.
“Sioni ni kwa msingi gani ujambazi ukifanywa jijini Nairobi na wachache ambao wanajulikana sasa, inakuwa ni kila mtu nchini anayejumlishwa kuwa mkora. Hakuna haja ya kutekeleza adhabu inayolenga bodaboda kote nchini,” akasema Bw Kinuthia.
Bw Kinuthia alisema kwamba licha ya kuwa anaunga mkono Rais Kenyatta na sera zake “kwa hili naomba kupinga.”
Mwenyekiti wa Madiwani wa Mlima Kenya Bw Charles Mwangi alisema kwamba Rais Kenyatta amenoa kiuchumi na kisiasa kuhusu amri hiyo dhidi ya Bodaboda.
“Adhabu aliyoamrisha kitaifa imesambaratisha riziki ya wengi wa vijana ambao ndipo walishe familia au wajilishe wenyewe, ni lazima bodaboda zao zifanye biashara ya uchukuzi. Walionaswa na polisi na pikipiki zao kufungiwa, wanadaiwa ama mlungula au faini kortini. Kisiasa, wapinzani wetu wameanza kutusuta kama walio na chuki dhidi ya walio chini kiuchumi. Tunapoteza ufuasi,” akasema Bw Mwangi.
Bw Mwangi ambaye anawania kiti cha ubunge cha Maragua kwa mrengo wa Azimio alisema kwamba adhabu hiyo ingewalenga tu walionaswa katika uhalifu huo wa Forest Road lakini pia maafisa wa polisi kichinichini wazindue msako dhidi ya wakora wanaojificha ndani ya sekta ya bodaboda.
Amri pana ya rais ni kwamba kila pikipiki inayohudumu kama ya uchukuzi wa umma isajiliwe na mamlaka ya uchukuzi na usalama wa ujumla unaozingatia ufaafu wa pikipiki, uhitimu wa mwendeshaji, bima ya abiria na uzingatifu wa sheria iwe ni lazima.
Tayari, Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi (DIG) Bw Edward Mbugua ametoa mwongozo kwamba wanabodaboda wasakwe kijumla na kila siku maafisa nyanjani wawe wakimtumia ripoti kuhusu idadi ya waliokamatwa, waliozuiliwa, walioshtakiwa, waliopigwa faini na kiwango gani na pia idadi ya pikipiki zitakazonaswa.
Wanasiasa wengi wamejitenga na hali hiyo huku katika maeneo mbalimbali nchini kukizuka makabiliano dhidi ya polisi na wahudumu wa pikipiki.