Karamu ya mbuzi yaokoa mshukiwa wa mauaji
NA BRIAN OCHARO
MWANAMUME aliyeshtakiwa kwa mauaji ameponea chupuchupu baada ya kujitetea kuwa damu iliyopatikana kwa nguo zake usiku wa mkasa ilikuwa ni ya mbuzi.
Kifungo cha kifo kimekuwa kikimkodolea macho Bw Nyundo Mwamuye baada ya kuhusishwa na mauaji ya kutisha ya Sidi Gowe Iha, aliyeuawa kwa madai ya uchawi.
Alijitetea kuwa, katika usiku wa mkasa, alikuwa na wenzake karamuni ambapo alihusika katika uchinjaji wa mifugo ndipo nguo zake zikawa na damu.
Kulingana naye, hakukuwa na uchanganuzi wa DNA uliotolewa mahakamani kuthibitisha alama za damu kwenye shati lake zinalingana na damu ya marehemu.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Mombasa Ann Ong’injo, aliyesikiliza kesi hiyo alikubaliana na Bw Mwamuye kwamba kutokana na kutokuwepo kwa uchambuzi wa DNA, ilikuwa vigumu kubaini iwapo doa la damu kwenye shati lake lilikuwa la mwanamke aliyeuawa au mbuzi ambao walikuwa wamechinja usiku huo.
Hakimu pia alibainisha kuwa huo ndio ushahidi pekee ambao ungeweza kumuunganisha mshtakiwa na kosa hilo kwa vile alikana kumuua mwanamke huyo.
“Mshtakiwa amepatikana hana hatia na anaachiliwa ipasavyo,” alisema Jaji huyo.
Jaji Ongi’njo alisema kushindwa kwa mpelelezi kupeleka shati hilo lililokuwa na damu kwa Maabara ya Serikali kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini uhusiano kati ya damu kwenye shati la mshtakiwa na marehemu ulidhoofisha kesi ya upande wa mashtaka.
Kesi kuhusu mauaji hayo ilianza mwaka wa 2018 alipokamatwa baada ya nguo zake kukutwa na madoa ya damu ambayo polisi walichukulia kama ushahidi uliomhusisha na mauaji hayo.
Hata hivyo, Bw Mwamuye alijitetea kwamba alikuwa miongoni mwa wanakijiji walioshiriki katika kuchinja mbuzi sita na ng’ombe wawili usiku ule ule ambao mwanamke huyo aliuawa.
Sherehe hiyo ilifanyika mnamo Septemba 8, 2018, kama kumbukumbu ya kifo cha marehemu mjombake.
Kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, mshukiwa pamoja na wenzake walichinja mifugo hiyo usiku kucha kabla ya kuingia ulevini wakicheza nyimbo za kitamaduni huku wakisubiri kuandaliwa chakula.
Wakiwa wanacheza, walipokea habari za kuuawa kwa mwanamke huyo, ambaye nyumba yake ilikuwa umbali wa takriban mita hamsini kutoka kwa boma la mjombake mshukiwa.
Chifu Msaidizi wa eneo hilo, Bw Sammy Baya, ambaye aliarifu polisi kuhusu tukio hilo la mauaji alimhusisha Bw Mwamuye na mauaji hayo kwa sababu alionekana akiwa amevalia shati lililokuwa na damu.
Mahakama iliambiwa mshukiwa alilibadilisha nguo baada ya kupata taarifa za mauaji.
Shahidi huyo pia aliieleza mahakama kuwa marehemu alidaiwa kuwa ni mchawi na ikadaiwa kuwa alimroga mtoto aliyefariki kijijini hapo.
Inspekta Ibrahim Bonaya aliyechunguza kesi hiyo alisema alimkamata mwanamume huyo kwa sababu alionekana akiwa amevalia shati lenye madoa ya damu asubuhi ya baada ya usiku ya tukio.
Kulingana na afisa huyo, mshukiwa huyo alitoa taarifa za kutatanisha kuhusu chanzo cha damu kwenye shati lake.
“Mshtakiwa alidai kuwa madoa ya damu yalitoka kwa mnyama ambaye alikuwa amechinja asubuhi hiyo na pia kudai kuwa pua yake ilitoka damu,” alisema Bw Bonaya.
Katika utetezi wake, Bw Mwamuye alikana kutenda kosa hilo. Alieleza kuwa alikuwa miongoni mwa waliokuwa wakichinja wanyama hao.
“Nilikunywa pombe usiku huo, nilianguka chini ambapo mifugo ilikuwa imechinjwa na hapo ndipo shati langu lilipata madoa ya damu,” alisema.
Aliongezea kuwa hakumjua marehemu wala kuingia nyumbani kwake usiku huo kwani alikuwa amelewa chakari.