ZARAA: Mbolea ya kiasili inavyosaidia kumudu gharama ya kilimo
NA LABAAN SHABAAN
BEI ya fatalaiza Kenya imepanda kutoka Sh4,000 hadi takriban Sh6,500 kwa gunia la kilo 50, huku mzozo unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine, ukiibua hofu kuu miongoni mwa wakulima, kwa kuwa ndio tegemeo la fatalaiza.
Mwaka jana, Urusi, ilikuwa namba moja duniani katika mauzo ya fatalaiza na vikwazo vya kibiashara dhidi yake vimeathiri kilimo duniani.
Hali si hali 2022 huku Wizara ya Kilimo ikihofia bei itapanda hadi Sh 7,000.
Fred Munene ambaye ni mkulima wa matikitimaji, pilipili hoho na butternuts eneo la Mwea Kaunti ya Kirinyaga, pia hutoa mafunzo kwa wakulima.
Fred Munene aonyesha zao la tikitimaji shambani mwake Mwea, Kirinyaga. PICHA | LABAAN SHABAAN
Anaeleza kuwa bei ya fatalaiza sasa inampa mafadhaiko.
“Kupanda kwa bei ya fatalaiza kumenishtua! Nimekuwa niking’ang’ana kupata faida hata kwa bei ya awali. Nimelazimika kupunguza matumizi ya shamba kutoka ekari 10 hadi nne ili nimudu gharama ya kuendeleza kilimo. Na kama bei sokoni itakuwa chini, nitabwagwa nje ya kilimo,” Munene anasema kwa masikitiko.
Katika harakati za kubaini iwapo wakulima wanaweza kuwa na njia mbadala ya kuendeleza kilimo chao kwa gharama nafuu, Akilimali ilizuru Lishe Demo Farm katika Kaunti ya Kiambu eneo la Kikuyu.
Lishe Demo Farm, ni shamba la ekari tatu la mazao ya kiasili. Mazao yapandwayo humu hutumia mbolea. Kituo hiki kadhalika huandaa mbolea na kufunza wakulima jinsi ya kuitengeneza na vile vile kuwauzia.
Hosea Munene Mugera, mwasisi wa Lishe Demo Farm, alianza kilimo 2003 alipokuwa anapanda nyanya. Baada ya bei za fatalaiza na dawa za vimelea kupanda na kuwa hatari kwa ubora wa udongo, aliamua kukumbatia kilimo asili mwaka 2008. Ili aelewe vyema, Mugera alienda shuleni kujifunza kilimo asili.
Kila miezi mitatu, Lishe Demo Farm huzalisha tani 20 za mbolea. Kumi huuzwa kwa wakulima wengine na kumi hutumika katika upanzi shambani mwake. Mugera huuza mfuko wa mbolea wa kilo 50 kwa Sh500 ambacho ni kiasi kidogo kikilinganishwa na bei ya fatalaiza. Hivi karibuni anapanga kuongeza wafanyakazi wa kuandaa mbolea kwa sababu wateja wanaongezeka.
“Ili utengeneze mbolea unahitaji matawi, nyasi, karatasi, majani, magugu, taka kutoka kwa mifugo, mchanga, majivu, maji na taka za jikoni. Malighafi hii yote inapatikana katika mazingira tunamoishi. Kama si kupata bure mimi hununua kinyesi cha mifugo kwa bei ya chini,” Mugera anasema.
Shambani mwa Mugera kuna kila kitu anachohitaji kuunda mbolea. Anatuambia kuwa ili apate madini ya nitrojeni, hutumia kinyesi cha kuku, mbuzi, ng’ombe na kadhalika. Nitrojeni husaidia mmea kuwa na matawi yenye afya.
Vile vile, ili kuhakikisha ana madini ya Phosphorus na Potassium ambayo hunawirisha maua, matunda na mizizi ya mimea, hutumia kinyesi cha sungura na farasi.
“Tunalinda afya ya mimea yetu na mazao kwa njia mbili. Njia ya kwanza ni kutumia mbolea kwa njia mwafaka kuzuia magonjwa kwa mimea kupitia mchanga na ya pili ni kuzuia wadudu, bila kuwaua, wasiathiri mimea. Tunawafukuza wadudu shambani kwa kupanda mimea yenye harufu kali ili wasikaribie mazao,” anaongeza.