DOMO: Kheri msela na Kizungu chake cha kuboronga!
NA MWANAMIPASHO
KUNA msemo choka mbaya usemao, ‘debe tupu halikosi kelele’.
Japo ni semi iliyotumiwa kwa miaka na mikaka, uzito wa maana yake upo pale pale.
Hivi umewahi kulipiga teke debe la bati lisilokuwa na kitu ndani? Kitakachofuatia ni wewe kuyaziba maskio kujilinda dhidi ya kero ya kelele itakayotokana na tukio hilo. Ndivyo wengi wenu nimegundua mlivyo mitandaoni.
Wikendi iliyopita ilibamba sana kwa wengi wetu wapenda sinema.
Kwa mara ya kwanza tulipata kushuhudia ‘Reality Show’ yenye asilimia mia ya uasili wa Kiafrika.
Shoo hii ilikwenda kwenye levo moja na zile za majuu kama Love Island, Too Hot To Handle, Love & Hip Hop Atlanta kati ya nyinginezo. Nazungumzia Young, Famous & African iliyowakusanya mastaa kadhaa maarufu wa Showbiz katika bara letu hili.
Ubora na kiwango cha shoo ndio sababu ilitrendi Kenya, Afrika Kusini, Nigeria na Uganda. Sijui kwa nini haikutrendi Tanzania, licha ya kuwa na mhusika mkubwa kutoka huko Diamond Platnumz.
Ila nataka kuamini ni kwa sababu wenzetu kule bwana Kizungu bado ni kizungumkuti.
Kama kuna kitu kimoja ninachoamini tunakubaliana nacho kwa pamoja ni kwamba shoo ilikuwa kali.
Mwenyewe niliitizama Season nzima kwa usiku mmoja. Nashukuru usingizi Jumamosi hiyo iliyotoka, uliamua kuyapa macho yangu nafasi. Kwa yale matukio, ilikuwa ni lazima ingetrendi.
Kusema kweli kupitia Hashtag kibao zilizoibuka kwa kutegemea mhusika mlengwa, komenti zilikuwa za kuchekesha sana.
Zile komenti kwangu mimi nilizitafsiri kuwa ni mapokezi mazuri ya shoo ile.
Mgala muuwe lakini haki yake mpe. Kwa mpenzi wa showbiz, ile ilikuwa kiboko. Tena ukizingatia kwamba ina ukaribu na nyumbani hata kama Kenya tulikosa mwakilishi, kwa kweli ngoma iliweza.
Pamoja na komenti zenu kibao, zilizonichukiza zaidi ni zile za wale walioamua kumtoa rangi Diamond na Kiingereza chake cha kuboronga. Hawa ndio zile debe tupu niliotangulia kuelezea.
Yaani kwenye shoo nzima kitu cha pekee baadhi yenu mlichokiona ni kizungu cha wasiwasi cha msela. Mwanzo kabisa mimi nampa tano sababu bwana kajitahidi. Siku hizi kizungu chake afadhali kuliko miaka ya nyuma. Ndio bado hayuko sawa ila kwa asilimia 100, hata nyie mazuzu mliokuwa mnamchamba nina uhakika mtampa asilimia 80.
Inasikitisha kwamba mpaka sasa tumegoma kabisa kuienzi na kuitukuza lugha yetu asilia ya Kiswahili. Tunaona ni sifa sana kujua Kiingereza. Ndio maana shoo haikutrendi Tanzania sababu wale bwana licha ya kutawaliwa na mbeberu Mjerumani, hicho Kijerumani ndo 90% hawakijui.
Sasa utamtegemeaje Diamond kukielewa Kizungu? Hivi upo sawa kweli? Kizungu anachokifahamu msela kinatosha. Kinatosha kumsaidia kuomba maji ya kunywa, kuwasiliana anaposafiri katika nchi za wenyewe. Hiyo inatosha.
Hivi mbona huwa hatuwacheki na kuwasimanga Wazungu wanapochemsha wanapokuwa wakizungumza Kiswahili? Halafu kwa nyie mnaoona kuifahamu lugha hiyo ya wenyewe ndio ustaarabu, basi mtabaki kuwa madebe tupu sababu hamna lingine la kujitambia nalo zaidi ya lugha ya wenyewe.
Kheri msela, juzi alikuwa anahangaika ghetto kule Tandale leo anatesa na kina Snoop Dogg na kizungu chake hicho cha kuunga unga.
Leo anaishi kwenye kasri lake. Anasukuma Rolls Royce wakati wewe hapo hata baiskeli ya Black Mamba huna. Ulichonacho tu ni bando za Shilingi 100 za kumkejeli jamaa Twitter.
Mjomba eeh, Shangazi eeh, upo vibaya sana ujue. Unahitaji uchunguzi wa kisaikolojia nakwambia!
Next article
Ulaya yaililia Afrika iiunge kulaani hatua ya Urusi…