[ad_1]
Diwani Guyo apatwa na msiba
Na COLLINS OMULO
KIONGOZI wa wengi katika Bunge la Kaunti ya Nairobi Abdi Guyo amepoteza watu wanne wa familia yake kupitia ajali mbaya ya barabarani.
Hata hivyo, wengine wawili walinusurika katika ajali hiyo iliyotokea walipokuwa wakisafiri kutoka Nairobi kwenda Isiolo Jumatatu, Machi 28, 2022. Waliokufa ni pamoja na kakake Guyo, mke wa kaka yake na wanao wawili. Watoto wengine wawili walinusurika.
“Walikuwa wakisafiri kutoka Nairobi kuelekea Isiolo na walikuwa kilomita chache kutoka kabla ya ajali hiyo kutokea,” akasema Diwani wa Wadi Kariobangi South Robert Mbatia, ambaye ni rafiki wa karibu wa Bw Guyo. Kisa hicho kimejiri siku chache baada ya Gavana wa Isiolo Mohamed Kuti kujiondoa kutoka kinyang’anyiro cha ugavana na kumpendekeza Bw Guyo (ambaye ni Diwani wa Matopeni, Nairobi) kuwa mrithi wake. Gavana huyo alisema kuwa amejiondoa kutokana na matatizo ya kiafya.
“Nimejiondoa kutoka mikimbio ya kutetea kiti changu kutokana na changamoto za kiafya,” Dkt Kuti akasema baada ya kukutana na viongozi pamoja na wazee kutoka ukoo wa Sakuye mjini Nanyuki Ijumaa wiki jana. Gavana huyo hajaonekana hadharani kwa miezi mitatu, tangu Desemba 2021.
Dkt Kuti alisema Bw Guyo ambaye alikuwa ametangaza azma ya kuwania kiti cha ubunge cha Embakasi ya Kati, ndiye anayefaa kujaza nafasi hiyo. Kwa upande wake Bw Guyo alikaribisha kuidhinishwa kwake akisema atawania kiti cha ugavana wa Isiolo kwa tiketi ya chama cha Jubilee. “Naamini niko na uwezo, nguvu na ujuzi wa kuinua kaunti yetu hadi ifikie upeo wa maendeleo,” Diwani huyo akaeleza.
Bw Guyo sasa atapambana na Gavana wa zamani Godana Doyo, aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Halakhe Waqo na mwanasiasa Hussein Tene.
Next article
Diwani Guyo apatwa na msiba
[ad_2]
Source link