Msimamizi akosoa miradi hewa kwenye kaunti
NA KENNEDY KIMANTHI
SERIKALI za kaunti zinaendelea kutumia mamilioni ya pesa kwa miradi hewa na mingine isiyotimiza viwango vya ubora unaostahili, kwa mujibu wa ripoti ya Msimamizi wa Bajeti.
Ukaguzi wa miradi iliyotekelezwa katika kaunti nyingi nchini ulibaini kuwa, baadhi ya miradi ni mibovu kwa sababu ilijengwa vibaya ilhali waliopewa kandarasi walilipwa.
Msimamizi wa Bajeti, Dkt Margaret Nyakang’o, ametaka kaunti ziboreshe mbinu za kusimamia, kufuatilia na kutathmini miradi ili kuhakikisha pesa za umma zinatumiwa vyema.
Katika ripoti yake kuhusu utekelezaji wa bajeti katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka wa kifedha 021/2022, Dkt Nyakang’o anasema baadhi ya miradi imekwama huku mingine ikirudiwa na hivyo haisadii umma kwa njia yoyote.
“Katika kipindi hicho, tulifanya tathmini katika kaunti tukitathmini miradi ambayo ilitekelezwa kipindi cha 2018/19 na 2019/20,” alitanguliza katika ripoti hiyo.
“Ilibainika hapakuwa na mbinu bora ya kusimamia miradi na hivyo kukawa na utekelezaji duni,” akaeleza.
Ripoti hiyo imetokea wakati ambapo wanasiasa nchini wamekuwa mbioni kutangaza uzinduzi wa miradi chungu nzima Uchaguzi Mkuu unapojongea.
Katika Kaunti ya Kilifi, ilibainika baadhi ya miradi haijafanikiwa kutimiza malengo yaliyonuiwa kwa sababu kuna miradi ambayo haijakamilika, mingine imekwama na kuna inayokumbwa na changamoto nyinginezo.
Mifano iliyotajwa ni ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza bidhaa za mihogo katika Kaunti Ndogo ya Kilifi Kaskazini, na bustani ya umma ya Malindi Water Front.
Kaunti ya Lamu ilikosolewa kwa ujenzi wa kitengo cha kutibu wagonjwa wasiolazwa katika hospitali ya Mpeketoni, ilhali kitengo hicho hakina vifaa wala wahudumu, na hivyo hakiwezi kutolea wananchi huduma.
Kwingineko Tana River, ripoti hiyo inasema ujenzi wa kituo cha kupima uzani wa magari ya kusafirisha mizigo katika eneo la Bangale, na kitengo cha matibabu ya dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Hola zinahitaji hatua za haraka kutoka kwa Serikali ya Kaunti ili ujenzi ukamilike na matumizi yaanze.
Katika Kaunti ya Kitui, miradi ilichelewa kukamilika kwa sababu wajenzi waliopewa kandarasi hawakulipwa.
Nayo Serikali ya Kaunti ya Laikipia ilikosolewa kwa kutopeleka walimu waliohitimu na vifaa vya kielimu vinavyohitajika katika shule anuwai zilizojengwa kwa pesa za umma.Kaunti ya Machakos haikubaki nyuma, kwani ilipatikana kuna miradi iliyojengwa kwa njia duni.
Miradi hiyo inajumuisha zahanati ya Mukunike iliyo Kangundo, darasa la chekechea lililo katika Shule ya Msingi ya Kinanie, Mavoko, na daraja la wapitanjia la Kwa Nzomo lililo Athi River.
“Zaidi ya hayo, kulikuwepo miradi iliyokwama katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo hasa kutokana na kutolipwa kwa wajenzi,” ikaeleza ripoti hiyo.
Kaunti nyingine zilizopatikana na miradi isiyosaidia ni Baringo, Bomet, Elgeyo Marakwet, Marsabit, Embu, Meru, Nandi, Nyamira, na Kisii.
Hata hivyo, ripoti hiyo ilitaja pia miradi ambayo imetekelezwa vyema katika kaunti nyinginezo na hivyo kuleta afueni kwa umma.
Kwa mara nyingine, Kaunti ya Makueni ilitajwa kama mfano bora ambapo serikali ya kaunti hutumia maoni ya wananchi katika utekelezaji wa miradi inayonufaisha umma.
Mfano wa miradi iliyochunguzwa Makueni ikapatikana kuwa bora ni mradi wa usambazaji maji wa Kyakithuku ambao unanufaisha vijiji vitatu vilivyoko katika Wadi ya Ilima.
Kaunti hiyo pia ilipatikana kutekeleza vyema ujenzi na utumiaji wa kiwanda cha kutengeneza lishe ya ndege, ambacho huwasaidia sana wafugaji wa ndege, mbali na ustawishaji wa kilimo cha parachichi na makadamia katika eneo la Mukaa.
Kaunti nyingine zilizopatikana kuwa na miradi bora ni Tharaka Nithi ambapo ununuzi wa mtambo wa kuchimba visima ulileta manufaa kwa wananchi, na Trans Nzoia ambapo kulibainika ujenzi unaoendelea wa Hospitali ya Rufaa ya Trans Nzoia unaotekelezwa ipasavyo.
Katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, kuna baadhi ya miradi iliyotekelezwa vyema kama vile ujenzi wa darasa jipya la chekechea katika Shule ya Msingi ya Sitoton, ambao ulisemekana kuongeza idadi ya wanafunzi kwa asilimia hamsini.
Next article
Murang’a yaibuka kitovu cha siasa Mlima Kenya