Polisi wamechoka na siasa za mapema, Matiang’i alalamika
NA MARY WANGARI
WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i amesema kuwa kampeni za mapema zinazoendelezwa na wanasiasa wakuu kote nchini zimewachosha maafisa wa polisi.
Waziri Matiang’i, kupitia taarifa yake, alilalamika kuwa kampeni hizo zimekuwa mzigo kwa polisi na taasisi nyinginezo za ulinzi kutokana na idadi kubwa ya maafisa wanaotumwa kukabiliana na ghasia zinazohusiana na mikutano ya kisiasa.
Kulingana na notisi rasmi iliyochapishwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati, kampeni za Uchaguzi Mkuu zinastahili kuanza rasmi Mei 29 hadi Agosti 6.
“Kipindi cha kampeni kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 kitaanza Jumapili Mei 29 na kukamilika Jumamosi, Agosti 6, 2022, saa 48 kabla ya Siku ya Uchaguzi Mkuu. Muda wa kampeni utaanza saa moja asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni wakati wa kipindi hicho cha kampeni,” kinasema kijisehemu cha notisi kutoka IEBC.
Licha ya notisi hiyo, viongozi kadhaa wa kisiasa wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, wamekuwa wakizunguka kaunti mbalimbali kila wikendi katika juhudi za kuwashawishi wapigakura kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopangiwa kufanyika Agosti 9.
Dkt Matiang’i sasa ameitaka IEBC kutekeleza vikali maagizo kuhusu kalenda ya uchaguzi hasa kuhusiana na kipindi rasmi cha kampeni akisema hali ya kupiga siasa kwa muda mrefu inaathiri kiasi uchumi wa kitaifa na familia.
Isitoshe, alifafanua kuwa mjadala shirikishi kuhusu sheria za uchaguzi na kanuni kuhusu matumizi ya pesa za siasa, uliopaswa kudhibiti matumizi ya wanasiasa, vilevile unachochea ghasia kuhusu kugawanya pesa za hongo miongoni mwa umma unaokusanyika kwenye kampeni hizo za kisiasa.
“Tumekuwa katika hali ya kupiga siasa kwa muda wa miaka minne iliyopita. Kinachofuata ni michafuko inayotokana na kutofautiana kuhusu jinsi ya kugawana rushwa za pesa za kampeni. Tumelazimika kutenga raslimali zaidi ili kudhibiti halaiki za wafuasi ikiwemo fujo zinazozuka na suala hili limelemea raslimali tulizo nazo,” alisema Waziri Matiang’i.
Alisema timu inayojumuisha polisi na mashirika mengineyo ya ulinzi imetumwa katika maeneo yanayotazamiwa kuwa na ushindani mkali kabla ya teuzi za mchujo za vyama vya kisiasa zinazotazamiwa kuanza katika muda wa wiki mbili zijazo na kukamilika Aprili 24.
Akizungumza katika kikao na Baraza la Madhehebu Mbalimbali Nchini (ICRK) Waziri alisema kando na kikosi hicho maalum, serikali pia imeimarisha doria kuhusu shughuli za kisiasa na msako dhidi ya wanasiasa wanaoneza chuki na matamshi ya uchochezi.
Next article
Afueni serikali ikipunguza pakubwa bei za mbolea