[ad_1]
Villarreal yaduwaza Bayern Munich katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali ya UEFA
Na MASHIRIKA
FOWADI wa zamani wa Bournemouth, Arnaut Danjuma alifunga bao la pekee lililowawezesha waajiri wake Villarreal kuduwaza Bayern Munich kwenye mkondo wa kwanza wa robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumatano usiku nchini Uhispania.
Ilikuwa mara ya kwanza tangu 2017 kwa Bayern kupoteza mechi ya UEFA ugenini.
Villarreal waliokuwa wakichezea nyumbani, walianza mechi kwa matao ya juu na kuonekana kuwazidi maarifa wageni wao katika takriban kila idara. Baada ya Danjuma kuwaweka kifua mbele katika dakika ya nane, Farncis Coquelin alifungia Villarreal bao la pili ambalo halikuhesabiwa huku Gerard Moreno alishuhudia kombora lake likibusu mwamba wa lango la Bayern.
Bayern ambao ni miamba wa soka nchini Ujerumani hawakushambulia wenyeji wao katika kipindi chote cha kwanza huku wakielekeza makombora matatu pekee langoni mwa Villarreal katika kipindi cha pili.
Kigogo Robert Lewandowski ambaye amefungia Bayern na timu ya taifa ya Poland mabao 51 kufikia sasa msimu huu alikosa kuridhisha katika safu ya mbele ya waajiri wake. Alikabwa vilivyo na mabeki wa Villarreal walioendeleza ubabe uliowawezesha kung’oa Juventus katika hatua ya 16-bora ya UEFA msimu huu.
Licha ya kutoridhisha katika mchuano wa mkondo wa kwanza, Bayern bado wanapigiwa upatu wa kufuzu kwa nusu-fainali za UEFA msimu huu. Watarudiana na Villarreal ya kocha Unai Emery uwanjani Allianz Arena mnamo Aprili 12, 2022.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO
[ad_2]
Source link