Manchester United sasa waamua kocha wao mpya atakuwa Erik ten Hag wa Ajax
Na MASHIRIKA
MANCHESTER United wamefichua kwamba kocha wa Ajax, Erik ten Hag ndiye ataachiwa mikoba yao ya ukufunzi baada ya Ralf Rangnick kuondoka mwishoni mwa msimu huu wa 2021-22.
Mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wamekuwa wakitafuta kocha mrithi wa Ole Gunnar Solskjaer na wamekuwa wakihusishwa pakubwa na Ten Hag na mkufunzi wa zamani wa Tottenham Hotspur ambaye sasa anadhibiti mikoba ya Paris Saint-Germain (PSG), Mauricio Pochettino.
Wawili hao walipiku Thomas Tuchel wa Chelsea, Luis Enrique wa timu ya taifa ya Uhispania na Julen Lopetegui anayewanoa masogora wa Sevilla katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).
Kwa mujibu wa gazeti la Times nchini Uingereza, Ten Hag, 52, aliridhisha zaidi katika mahojiano aliyofanyowa na wasimamizi wa Man-United na anatarajiwa kutia saini mkataba atakaopokezwa wakati wowote kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kampeni za EPL muhula huu kupulizwa.
Inaaminika kuwa Ten Hag ndiye aliye na uwezo wa kuchangia uthabiti wa kikosi cha Man-United kinachosaka mtindo utakaokitambulisha katika ulingo wa soka.
Chini ya Ten Hag ambaye ni raia wa Uholanzi, Ajax kwa sasa wanatandaza soka safi ya kuvutia ambayo vinara wa Man-United wangependa iletwe ugani Old Trafford baada ya kushuhudia ukame wa mataji kabatini mwao kwa miaka mitano iliyopita.
Man-United walipoteza mtindo uliowatambulisha kimchezo chini ya wakufunzi David Moyes, Jose Mourinho, Louis van Gaal na Ole Gunnar Solskjaer walioaminiwa fursa za kudhibiti mikoba yao baada ya Sir Alex Ferguson kustaafu mnamo Mei 2013.
Wakinolewa na Ferguson, Man-United walicheza kwa kuonana na kushambulia sana – mbinu ambayo sasa ni kitambulisho cha Ajax chini ya Ten Hag aliyewahi pia kuwatia makali chipukizi wa Bayern Munich kati ya 2013 na 2015.
Tangu apokezwe mikoba ya Ajax mnamo 2017, Ten Hag aliongoza waajiri wake hao kutwaa taji la Eredivisie mnamo 2018-19 na 2020-21. Ajax pia walitinga nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2018-19 baada ya kudengua Real Madrid na Juventus. Safari yao ya kuwania ufalme wa kipute hicho ilikatizwa na Tottenham Hotspur.
Ajax wanaopigiwa upatu wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uholanzi kwa mara nyingine msimu huu, wanafahamika kwa mfumo wa 4-2-3-1 au 4-3-3 ambao pia umekumbatiwa pakubwa na Man-United muhula huu. Hata hivyo, udhaifu wao umechangiwa na kukosekana kwa kiungo mbunifu aliye na uzoefu wa kupakua pasi za hakika kwa kasi inayofaa.
Baada ya Atletico Madrid ya Uhispania kudengua Man-United kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA msimu huu, matumaini ya Red Devils kujinyanyulia taji lolote muhula huu yalizimika.
Kufikia sasa, Man-United wanashikilia nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 51 sawa na West Ham United. Ni pengo la alama tatu ndilo linawatenganisha na Spurs wanaofunga orodha ya nne-bora.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO