Connect with us

General News

Matajiri watesa maskini kwa ulafi – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Matajiri watesa maskini kwa ulafi – Taifa Leo

Matajiri watesa maskini kwa ulafi

NA PETER MBURU

KAMPUNI kubwa za kuuza mafuta nchini zimemulikwa kwa kuyafungia na kuwasababishia Wakenya mateso, licha ya kuwepo kwa wingi kwa bidhaa hiyo nchini.

Hii ni kutokana na hali ya kuendelea kukosekana kwa mafuta katika vituo vya kampuni kadhaa katika maeneo tofauti ya nchi, huku maelfu ya watu wakitafuta bidhaa hiyo bila mafanikio na wengine wengi kutatizika kiusafiri na kikazi.

Habari kutoka kwa Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi nchini (Epra) zinaonyesha kuwa licha ya vituo vya mafuta vya baadhi ya kampuni kukosa bidhaa hiyo, kampuni zenyewe zina shehena ambazo hazijachukua kutoka vituo vya kuhifadhi mafuta vya kampuni ya Kenya Pipeline, katika maeneo tofauti ya nchi.

Kulingana na Epra, kulikuwa na lita milioni 212 za petroli na lita milioni 188 za dizeli nchini kufikia Alhamisi wiki iliyo – pita, lakini kiwango cha chini cha mafuta yanayouzwa kikafanya mauzo ya kila siku kuwa chini ya lita milioni tisa na nusu.

Kampuni za Rubis, Total na Ola zinaongoza katika sakata hii inayoendelea kuwapitishia Wakenya wengi katika mateso kwa wiki ya pili, licha ya kuwa na usemi mkubwa katika biashara ya mafuta nchini, zikishikilia takriban robo ya soko la mafuta.

Kampuni hizi zina vituo vya mafuta katika kona tofauti za nchi na zimekuwa zikihudumia maelfu ya Wakenya kila siku, lakini kukosekana kwa bidhaa hiyo katika vingi vya vituo vyao kumewafanya Wakenya wengi kusumbuka.

Epra, hata hivyo, ilisema kuwa Total na Rubis kwa pamoja zilikuwa na lita milioni 1.59 za petroli na milioni 4.43 za dizeli jijini Nairobi kufikia Alhamisi.

Kampuni ya Ola nayo ilikuwa na lita milioni 1.25 za petroli na milioni 8.3 za dizeli Nairobi na Mombasa.

Lakini katika baadhi ya vituo vya mafuta vya Ola Nairobi, Bomet, Migori na maeneo mengine nchini hakukuwa na mafuta, vingi vikisalia kufungwa.

Vingi vya vituo vya Total vile vile vilikuwa vitupu, baadhi ya maeneo yaliyoathirika yakiwa Nairobi, Nanyuki na Kisii, sawa na vituo vya Rubis ambapo ni kimoja tu katika jiji la Nairobi ambapo lori la mafuta lilishuhudiwa likiwasilisha bidhaa hiyo.

“Tunawaomba wateja kutafuta mafuta mahali kwingine wanapokuja kwa kuwa hatujawa nayo,” akasema mhudumu katika kituo kimoja cha mafuta cha Total Nairobi.

Kwa pamoja, Total (16.4) na Rubis (8.6) zinamiliki asilimia 25 ya soko la mafuta nchini, zikifunga idadi ya tatu bora kati ya kampuni kubwa za mafuta baada ya Vivo Energy inayomiliki asilimia 21.7 ya soko.

“Walikuwa wakilaumu ukosefu wa malipo kuwa ndio umepelekea kukosekana kwa mafuta lakini walilipwa wiki iliyopita. Kwa nini sasa hawauzi?” afisa wa ngazi ya juu katika wizara ya Mafuta ambaye alilaumu kampuni hizo kuwa zinakosa kuuza kimakusudi, akasema.

Waziri wa Fedha, Ukur Yatani, wiki iliyopita pia alilaumu kampuni za kuuza mafuta kuwa zinayafungia ili kusababisha janga nchini, akisema tatizo kuu halikuwa malipo.

Lakini kuna tuhuma kuwa kampuni hizo zinakosa kuuza mafuta zikisubiri uhakiki wa bei mpya za mafuta nchini zitakazotangazwa Alhamisi, ambapo inasubiriwa kuwa zitapandishwa, kisha ziuze kwa faida ya juu.

“Kampuni kubwa za mafuta ndizo zinabeba uzito na zimejipata kwenye hasara kwa kuwa tayari zinauza shehena za Machi, ambazo bei yake inafaa kutangazwa Aprili,” akasema Katibu katika wizara ya Mafuta, Andrew Kamau wiki iliyopita.

Taifa Leo jana baada ya kubaini kuwa vingi vya vituo havikuwa na mafuta licha ya kuwa kuna shehena, iliwatafuta maafisa wakuu wa kampuni za Rubis na Total, pamoja muungano wa kuwawakilisha ili kufafanua sababu ya hali hiyo, lakini wote hawakupokea simu wala kujibu jumbe fupi zilizotumwa kwa simu zao.