Klopp aingia nusu fainali UEFA
Na MASHIRIKA
NDOTO ya Liverpool kujizolea jumla ya mataji manne msimu huu yalisalia hai baada ya kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp kudengua Benfica ya Ureno kwenye robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa jumla ya mabao 6-4.
Liverpool waliosajili ushindi wa 3-1 katika mkondo wa kwanza, waliambulia sare ya 3-3 katika marudiano yaliyofanyika ugani Anfield mnamo Aprili 13, 2022.
Beki Ibrahima Konate aliwaweka Liverpool kifua mbele katika dakika ya 21 baada ya kushirikiana na Kostas Tsimikas. Ingawa Benfica walisawazisha kupitia kwa Goncalo Ramos katika dakika ya 32, Liverpool walirejea uongozini baada ya kufungiwa mabao mawili na Roberto Firmino katika dakika za 55 na 65.
Benfica walipata mabao mawili zaidi katika dakika za 73 na 81 kupitia kwa Roman Yaremchuk na Darwin Nunez waliomwacha hoi kipa Alisson Becker.
Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool sasa watavaana na Villarreal katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali za UEFA mnamo Aprili 27 kabla ya marudiano kuandaliwa nchini Uhispania mnamo Mei 4, 2022.
Villarreal ya kocha Unai Emery ilibanduliwa na Liverpool kwenye nusu-fainali za Europa League mnamo 2016. Ilijikatia tiketi ya nusu-fainali baada ya kubandua miamba wa Ujerumani, Bayern Munich, kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya sare ya 1-1 ugani Allianz Arena mnamo Aprili 12, 2022.
Nusu-fainali ya UEFA kati ya Liverpool na Villarreal itakutanisha kocha Klopp na Emery anayejivunia kunyanyua mataji manne ya Europa League.
Matatu kati ya mataji hayo yamenyanyuliwa na Klopp akiwatia makali vijana wa Sevilla waliokomoa Liverpool kwenye fainali ya 2016. Alizoa taji jingine la kivumbi hicho mnamo 2020-21 kwa kuongoza Villarreal kukomoa Manchester United kwa penalti 11-10 baada ya sare ya 1-1 mnamo Mei 26, 2021.
Baada ya kumenyana na Manchester City kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA ugani Wembley mnamo Machi 16, 2022, Liverpool watamenyana na Man-United katika EPL mnamo Aprili 19, 2022 uwanjani Anfield. Waliambulia sare ya 2-2 dhidi ya Man-City katika mkondo wa pili wa EPL mnamo Aprili 17, 2022 uwanjani Etihad.
Iwapo watabandua Villarreal, basi Liverpool watafuzu kwa fainali ya UEFA kwa mara tatu kutokana na misimu mitano iliyopita chini ya Klopp aliyefanyia kikosi alichokotegemea dhidi ya Benfica ugenini mabadiliko saba uwanjani Anfield mnamo Aprili 13, 2022.
Liverpool waliopiga Chelsea kwa penalti 11-10 baada ya sare tasa kwenye fainali ya Carabao Cup mnamo Februari 27, 2022, sasa wanakamata nafasi ya pili kwenye jedwali la EPL kwa alama 73, moja pekee nyuma ya viongozi na mabingwa watetezi Man-City. Ni mechi saba pekee zimesalia kabla ya kipute cha EPL msimu huu kutamatika rasmi.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO
Next article
Sijajiondoa, nitawania tiketi ya UDA ugavana Kiambu –…