Wadau wa utalii waonya wanasiasa dhidi ya kuzua vurugu wakati wa kura
NA WINNIE ATIENO
VIONGOZI wa kidini na wadau wa sekta ya utalii Mombasa, wameonya kuwa uchumi wa kaunti hiyo utakuwa katika hatari kubwa ikiwa wanasiasa watachochea vurugu kuelekea kwa uchaguzi wa Agosti 9.
Viongozi hao wametoa wito kwa wanasiasa kuhakikisha wanadumisha amani wakati wote wa kipindi cha uchaguzi.
Wakizungumza katika kikao na wanahabari, viongozi wa kidini waliwataka wanasiasa kukoma kugawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila au misingi yoyote ile inayoweza kuzua ghasia.
Walisema watawalaani wanasiasa wanaosababisha machafuko mjini Mombasa na kueneza ukabila kwenye kampeni zao.
Mwenyekiti wa Chama cha Utalii wa Pwani ya Kenya (KCTA), Bw Victor Shitakha alisema sekta ya utalii ni mojawapo ya biashara ambazo huathirika zaidi na ghasia ilhali ni tegemeo kubwa la uchumi wa Mombasa na Pwani kwa jumla.
“Kukiwa na amani, sekta yetu itakuwa shwari. Tunataka amani ndipo wawekezaji wa sekta ya utalii waendelee na biashara zao. Sekta hii hunoga wakati usalama umedumishwa na kuna utulivu,” aliongeza.
Aliwashutumu wagombea wa ugavana kwa kupuuza utalii akisema hakuna aliyefanya kikao na wawekezaji wa utalii kung’amua changamoto na namna watakabiliana nazo watakapochaguliwa mamlakani.
Sheikh Rishard Ramadhan, mwanachama wa Majlis Ulama (baraza la wasomi wa Kiislamu) tawi la Mombasa aliwasihi hasa wagombea ugavana kaunti hiyo kuwa mstari wa mbele kukemea uchochezi wa kisiasa.
“Tumeishi kwa amani na maelewano, tusikubali mwanasiasa alete mifarakano na uadui kwa sababu ya siasa. Hatutaki mizozo. Vijana wetu wasitumike kusababisha ghasia. Mombasa imekuwa na utulivu lakini baadhi ya wanasiasa wameanza kuhubiri siasa za chuki miongoni mwa vijana na kuwahonga,” alisema Sheikh Ramadhan.
Mhubiri Godfrey Nyongesa, aliwataka viongozi kufanya kampeni kwa utulivu.
“Hatutaki ukabila. Ukabila na migawanyiko ya kidini inayohubiriwa na baadhi ya wanasiasa ni hatari sana. Tunawasihi wakazi kudumisha amani. Tukumbuke Mungu ndiye atakayeamua kiongozi wetu atakuwa nani, jukumu letu ni kupiga kura na sio kupigana,” alisema Bw Nyongesa.