Connect with us

General News

Kwekwe abanwa kuhusu ukuta wa Sh24.9 milioni – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kwekwe abanwa kuhusu ukuta wa Sh24.9 milioni – Taifa Leo

Kwekwe abanwa kuhusu ukuta wa Sh24.9 milioni

NA DAVID MWERE

KATIBU wa idara ya urekebishaji tabia, inayosimamia kitengo cha magereza, Bi Safina Kwekwe, amemulikwa kuhusu kandarasi ya ujenzi wa ukuta uliogharimu Sh24.9 milioni katika gereza la Shimo la Tewa.

Mhasibu Mkuu, Bi Nancy Gathungu, alitilia shaka ujenzi wa ukuta huo wa mita 225 ambao ulibomoka punde baadaye.

Alitilia shaka pia kasi iliyotumiwa kupeana kandarasi hiyo katika mwaka wa kifedha wa 2020/2021 kwa kampuni ya Trans Border Enterprises bila kutangazwa.

Alipofika mbele ya Kamati ya Uhasibu wa Umma (PAC) akiandamana na Bi Kwekwe, Kamishna Mkuu wa Huduma za Magereza ya Kenya, Brigedia Mstaafu John Warioba, alikiri kuwa kuporomoka kwa ukuta huo ilikuwa suala zito lililohitaji kuingiliwa kati na Baraza la Kitaifa la usalama (NSC). Baraza hilo huongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Bi Kwekwe alikuwa ametarajiwa kuwa mgombea mwenza wa Prof Hamadi Boga, kwa shindano la ugavana Kwale lakini akafichua kuwa barua yake ya kujiuzulu serikalini ilikataliwa.

Kulingana naye, wakubwa wake katika idara hiyo iliyo chini ya Wizara ya Usalama wa Nchi inayosimamiwa na Waziri Fred Matiang’i, walimwambia kuna masuala aliyohitajika kukamilisha katika idara yake. Hata hivyo, hakubainisha ni masuala yapi hasa.

Stakabadhi zilizowasilishwa na Bi Kwekwe kuhusu kandarasi hiyo tatanishi zilionyesha kuwa, cheti cha kwanza cha malipo ya Sh16.95 milioni ilitolewa Mei 5, 2017 na ya pili ya Sh4.97 milioni ikatolewa Julai 2, 2017. Malipo ya tatu ya Sh2.64 yalitolewa Oktoba 10, 2017 mkandarasi akalipwa Juni 26, 2018.

“Baadaye iliripotiwa kuwa, mnamo Julai 24, 2018, mita 95 za ukuta uliporomoka na kusababisha majeraha kwa mlinzi mmoja,” ripoti ya mhasibu ikasema.

Ijapokuwa ujenzi ulirudiwa upya, ilibainika mkandarasi aliondoka wakati ujenzi ulipofika asilimia 60 pekee.

Stakabadhi zinaonyesha kuwa, kitengo cha magereza kilitilia shaka mara kwa mara ujenzi ulivyokuwa ukifanywa lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na idara ya urekebishaji tabia wala idara ya ujenzi wa miundomsingi ya umma.

Hali hii ilipelekea mita nyingine 130 za ukuta kubomoka mnamo Julai 25, mwaka uliopita.

Bi Kwekwe alikiri idara yake ilikosea kwa kupeana kandarasi bila kufuata kanuni lakini akaahidi kujitolea kufuata kanuni katika siku za usoni.

“Nilichoarifiwa na wenzangu ni kuwa gereza hilo lina wafungwa hatari sana ilhali kulikuwa na ukuta mmoja pekee,” akasema, akieleza sababu za kuharakisha utoaji wa kandarasi.

Mwenyekiti wa PAC, Bw Opiyo Wandayi, ambaye pia ni Mbunge wa Ugunja, alisema ushahidi uliopokewa kufikia sasa waashiria kuna sakata iliyolenga kufuja mali za umma.

“Hapakuwa na nia yoyote ya kujenga ukuta kwa maslahi ya usalama wa nchi, bali hii ilikuwa ni njia ya kusaidia watu kadha kupata pesa,” akasema Bw Wandayi.

Kamati iliambiwa kuwa, maafisa wa idara ya ujenzi wa miundomsingi ya umma kutoka Pwani hawakuhusika katika ujenzi wa ukuta huo na wale waliohusishwa walitoka Nairobi.

Mbunge wa Suna Magharibi, Bw Peter Masara, alitilia shaka maelezo kwamba utoaji wa kandarasi uliharakishwa kwa vile ukuta huo ni muhimu kwa usalama wa nchi, akiuliza kwa nini haikuchukuliwa kwa uzito uo huo wakati ukuta ulipoporomoka.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Trending