MITAMBO: Kifaa cha kukama ng’ombe chawafaa wenye mifugo wengi
NA RICHARD MAOSI
KIFAA cha kukama ng’ombe, mbuzi au ngamia almaarufu kama milking machine hurahisisha kazi ikizingatiwa kuwa mkulima anaweza akawakama zaidi ya mifugo watano kwa saa moja tu.
“Ishara tosha kuwa atafanikiwa kuendesha kilimo kwa njia ya kisasa na kwa wakati huo kupata tija zaidi kwa gharama nafuu,” anasema mtaalam wa mifugo na bidhaa zinazotokana na maziwa kutoka Chuo Kikuu Cha Egerton Nakuru, Gabriel Kwendo.
Mtaalam huyu anashauri wakulima kukumbatia mfumo huu ili kukinga mifugo yao dhidi ya mkurupuko wa maradhi yanayoathiri chuchu ya mastitis .
Maradhi haya hutokea mara nyingi shughuli ya ukamaji inapoendeshwa kwenye mazingira ambayo si safi.
Hii ndio sababu mtaalam huyu anahimiza utumizi wa kifaa hicho kwa kuwa hupunguza uwezekano wa mkamaji kuathiri maziwa au kiwele cha mifugo moja kwa moja.
Anasema ingawa wakulima wadogo mashambani bado wanapendelea kutumia mikono yao kukama, wenzao katika sekta ya ufugaji ng’ombe wa maziwa kwa madhumuni ya kibiashara wanatumia mitambo.
Alifichulia Akilimali kuwa itamlazimu mkulima kuwekeza pakubwa ili kununua kifaa hiki, maana faida zake huwa ni nyingi, hususan karne hii ambayo kazi nyingi za kilimo huendeshwa kidijitali.
Matumizi ya mtambo wenyewe huwa ni mepesi, maana mkamaji anatakiwa kuelekeza mtambo wa milking machine kwenye chuchu za ng’ombe.
Sehemu ya mbele ya mtambo wa milking machine ambayo huwa imechukua umbo la vikombe huunganishwa na chuchu za mifugo.
Isitoshe mtambo huwa umeunganishwa na paipu ambazo husafirisha maziwa hadi kwenye mtungi safi hatua chache kutoka kwa mifugo wake.
“Baada ya kuwasha stima kifaa huanza kukanda zile chuchu na hatimaye kufyonza maziwa, labda kwa dakika kumi tu na shughuli huwa imekamilika,” anaeleza.
Kwendo anaongezea kuwa kifaa cha milking machine kina uwezo wa kutambua endapo kiwango cha maziwa ndani ya chuchu huwa yamepungua na hapo mkulima amemaliza kukama.
Ili kupata picha kamili Akilimali ilizuru eneo la Lanet viungani mwa mji wa Nakuru, ambapo tulikutana na Mzee Francis Mwangi ambaye anafuga mseto wa ng’ombe kwa ajili ya maziwa.
Anasema ingawa gharama ya lishe ni ghali sana siku hizi, mkulima analazimika kujitahidi zaidi kupata maziwa ya kutosha , na hata ikiwezekana ajitengenezee malisho yenye virutubishi ili kuzalisha maziwa kwa wingi.
“Kwa sababu mimi ni mfugaji wa ng’ombe wengi , ninatumia kifaa cha milking machine, kwani kina uwezo wa kukama maziwa mengi kwa urahisi bila kuumiza chuchu za ng’ombe,” anaongeza.
Hata hivyo, mkulima huyo anaeleza kuwa katika hatua ya kwanza kabla ya kuanza kutumia kifaa hicho kikamilifu, lazima uzoeshe mifugo kuelewa jinsi kifaa kinavyotumika.
Lau sivyo mifugo inaweza kukosa utulivu na hata ikashindwa kutoa maziwa kutokana na mihemko mingi ambayo huenda itakuwa imeizonga.
Aidha Mwangi anaongezea kuwa mtaalam ambaye atakuwa amepatiwa jukumu la kukama ng’ombe lazima awe na elimu ya kutosha kuhusu tabia ya mifugo hususan bayolojia ya ukamaji.
Vile vile, anahimiza kuwa mfugaji achague kwanza mifugo ambayo huwa na tabia ya utulivu kuzoesha ng’ombe kutumia kifaa hicho.