Uhuru amalizana na Ruto
NA BENSON MATHEKA
UHUSIANO kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kwa mara nyingine ulionekana wazi kuwa umezorota ajabu kufuatia kauli kali alizotoa Rais na matukio yaliyoshuhudiwa Jumatano alipoongoza sherehe ya mwisho ya kitaifa akiwa mamlakani.
Kwa mara kwanza katika utawala wake wa miaka tisa wa Rais Kenyatta, Dkt Ruto aliondolewa kwenye mpangilio wa wazungumzaji katika sherehe ya kitaifa aliponyimwa nafasi ya kumkaribisha rais kuhutubu.
Ingawa uhusiano wa wawili hao ulidorora baada ya handisheki ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo 2018, ni Jumatano pekee ambapo Dkt Ruto alinyimwa nafasi ya kumwalika kiongozi wa nchi kuhutubia taifa katika maadhimisho hayo ya kihistoria.
Katika sherehe za Jumatano katika Uhuru Gardens, Nairobi, Rais Kenyatta alianza kusoma hotuba yake baada ya kutuza Wakenya waliochaguliwa na kamati ya tuzo za kitaifa kwa wajibu wao wa kipekee kwa nchi.
Hata alipokuwa akitambua wageni na viongozi mashuhuri kabla ya kusoma hotuba yake, Rais Kenyatta hakutaja jina la Dkt Ruto.
“Mheshimiwa Julius Maada Bio, Rais wa Sierra Leone, Mama Taifa wa Sierra Leone, Dkt Akiwumi Ayodeji Adesina- Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika, Waheshimiwa Maspika, Mheshimiwa Jaji Mkuu Martha Koome, viongozi wote wa kitaifa, Wakenya wenzangu, mabibi na mabwana, hamjambo,” alisalimu rais akianza hotuba yake.
Katika kile kilichoonyesha wazi kuwa uhusiano wao umeyeyuka kabisa, Rais Kenyatta alitoa kauli zilizoonekana kumponda Dkt Ruto moja kwa moja kwa kudai baadhi ya watu walinyakua ardhi ya umma ya uwanja wa ndege wa Wilson.
Aidha, alidai baadhi ya watu ni sumu kwa uongozi wa nchi kwa kuwa wana tabia ya kujifanya wazuri mbele ya umma.“Masuala ya ardhi hayakuwa yakishughulikiwa kidijitali, hivyo basi Wizara ya Ardhi ilikuwa pango la ufisadi. Sehemu ya uwanja wa ndege wa Wilson hapa ilikuwa imesajiliwa kwa jina ya mtu binafsi,” alisema Rais Kenyatta. Dkt Ruto amekuwa akikanusha kuwa alinyakua ardhi ambayo hoteli yake ya Weston imejengwa. Ardhi ilikuwa ya Mamlaka ya Safari za Ndege ya Kenya (KCAA).
Kwenye hotuba yake Rais Kenyatta alikemea Dkt Ruto kwa kudai kwamba, handisheki ililemaza miradi na mipango ya serikali.
“Ukweli ni kwamba, tumefanya mengi katika muhula wa pili kuliko muhula wa kwanza. Huu ndio ukweli mchungu ambao ni lazima wasikie na ambao hawawezi kuepuka,” akasema.
Katika mikutano yake ya kampeni za urais kuelekea uchaguzi mkuu ujao, Dkt Ruto amekuwa akidai handisheki ilivuruga mipango ya serikali na kulemaza Ajenda Nne Kuu.
Rais Kenyatta anaunga azima ya mpinzani mkuu wa Dkt Ruto, kwenye uchaguzi mkuu ujao Raila Odinga wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya. Na kwenye hotuba yake Jumatano, alitambua uteuzi wa kiongozi wa Martha Karua kuwa mwaniaji mwenza wa muungano huo.
“Ni matumaini yangu kwamba, Kenya itaweka historia kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa kuchagua naibu rais mwanamke,” alisema.
Kabla ya kuelekea Uhuru Gardens, Rais Kenyatta alikutana na mawaziri katika ikulu ya Nairobi lakini hakumwalika Dkt Ruto.
Afisi ya Dkt Ruto, kupitia afisa wa mawasiliano Emmanuel Talam ilisema kwamba, naibu rais hakualikwa kwenye hafla hiyo ambayo mawaziri waliitumia kumuaga Rais Kenyatta kabla ya kuongoza sherehe yake ya mwisho ya kitaifa.
Katika hatua iliyoashiria kuwa wafuasi wa Dkt Ruto walikasirika aliponyimwa nafasi ya kuhutubu, baadhi ya watu walianza kuondoka Uhuru Gardens, Rais Kenyatta alipoanza kusoma hotuba yake.
Hali ya kuyeyuka kwa uhusiano wa wawili hao ilionekana baada ya sherehe, Rais alipomkwepa Dkt Ruto.
Matukio ya Jumatano yalijiri siku sita baada ya Dkt Ruto kuomba msamaha Rais Kenyatta kwa makosa ambayo huenda alimfanyia.
Alisema haya wakati huo: “Pia ninajua kwamba, nikihudumu kama Naibu Rais, huenda nilifanya makosa ambayo hayakumfurahisha mkubwa wangu Mheshimiwa Rais, rafiki yangu mkubwa. Ninaomba msamaha.”
Dkt Ruto alikuwa amepanga mkutano wa kampeni Kiambu, kaunti ya nyumbani ya Rais Kenyatta baada ya sherehe za Madaraka Dei.