I
MZOZO wa uteuzi wa mwaniaji kiti cha Ugavana Kitui kwa tikiti ya chama cha Wiper ulitokota zaidi baada ya mahakama kuu kuharamisha ushindi wa Dkt Julius Malombe.
Jaji Christine Meoli aliyezamisha uteuzi wa Dkt Malombe alikiamuru chama cha Wiper kifanye uteuzi upya katika muda wa saa 72.
Jaji Meoli alikubaliana na aliyekuwa rais wa chama cha mawakili nchini (LSK) Erick Mutua kwamba sheria za uteuzi hazikufuatwa wakati wa kuchaguliwa kwa mwaniaji wa kiti cha Ugavana Kitui wa chama cha Wiper.
Ushindi wa Dkt Malombe, ambaye alikuwa gavana wa kwanza wa kaunti ya Kitui ulipingwa na Balozi Kiema Kilonzo.
Bw Kilonzo alilalamika Dkt Malombe alikabidhiwa cheti cha uteuzi kwa njia isiyokubalika kisheria.
Bw Kilonzo alisema mchujo ulifanywa kumteua atakayepeperusha bendera ya Wiper lakini “Dkt Malombe alipewa tikiti ya moja kwa moja.”
Jaji Meoli alitoa uamuzi huo kufuatia rufaa iliyowasilishwa na Bw Kilonzo aliyekuwa Balozi wa Kenya nchini Uganda.
Bw Mutua alieleza Jaji Meoli kwamba mfumo wa uteuzi ulibadilishwa baadaye na basi mchakato mzima ukaborongwa.
Bw Mutua alieleza mahakama kifungu nambari 38 kuhusu uteuzi kilikandamizwa.
Mahakama ilifahamishwa Bw Kilonzo hakupewa fursa ya kujitetea na kuwasilisha malalamishi yake.
“Sheria zinazotoa mwongozo wa kisiasa kwa vyama kuhusu uteuzi wa moja kwa moja zilikandamizwa na chama cha Wiper,” alisema Bw Mutua.