Mtangazaji wa Radio Citizen Jerida Andayi ambaye pia ni rafiki wa Ruth alikuwa wa kwanza kuuchapisha ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram akiwajulisha mashabiki kuhusu hayo.
Alipakia picha waliyopiga na Ruth huku wawili hao wakiachia tabasamu kutokana na habari hiyo njema kwa rafikiye ambaye mumewe aliaga dunia kutokana na mkasa wa gesi nyumbani.
“Hatimaye! Dadangu mdogo Ruth Matete ameruhusiwa kumzika mumewe. Mungu ni mwema,”Jerida alisema.
Wakati uo huo aliwarai watu kumsaidia Ruth katika kuandaa mazishi ya mumewe na kumchangia hela za kugharamia mazishi ya marehemu.
“Naomba tumpe Pasta Beloved John mazishi ya kiheshima kupitia nambari ya paybill ya 891300 Akaunti 39659. Shukran kwa sala zenu. Mambo yalikuwa magumu. Lakini Mungu amejidhihirisha,” aliongeza.
Haya yanajiri takriban mwezi mmoja baada ya Ubalozi wa Nigeria nchini Kenya kuamuru kuwa John asifanyiwe mazishi hadi serikali ya taifa hilo kutoa mwelekeo.
Awali TUKO.co.ke iliripoti kuwa Ruth alielekea mahakamani akitaka ubalozi wa nchi hiyo kugharamia bili ya makafani.
Kupitia kwa wakili wake Robert Odanga, mwimbaji huyo wa wimbo wa Nakupenda alisema kuwa gharama ya makafani inazidi kupanda licha ya maiti ya mumewe kupasuliwa na kubaini kilichomuua.
Kulingana na mjane huyo, familia ya mwenda zake ilimkubalia kumzika mumewe mwenye umri wa miaka 42 nchini Kenya.
John, mchungaji kutoka Nigeria alithibitishwa kuaga dunia Jumapili, Aprili 12, 2020 kufuatia mkasa mbaya wa gesi ambapo aliachwa na majeraha ya kuchomeka kwa asilimua 60.