Afueni serikali ikipunguza pakubwa bei za mbolea
Na WINNIE ONYANDO
WAKULIMA nchini wamepata afueni baada ya serikali kuwekeza Sh5.7 bilioni katika mpango wa mbolea. ya bei nafuu.
Waziri wa Kilimo, Peter Munya, alisema kuwa bei hizo mpya zitawapunguzia wakulima mzigo wa kutumia pesa nyingi kununua mbolea.
Akizungumza jana jijini Nairobi, Bw Munya alisema kuwa bei hizo mpya zitaanza kutumika kuanzia Jumamosi.
Tangazo hilo linajiri baada ya bei hizo kupanda kwa viwango vya juu kwa miezi 12 iliyopita. Bei hizo ziliathiri wakulima kwa kiasi kikubwa ikizingatiwa kuwa ndio huchangia utoshelevu wa chakula nchini kwa asilimia 100.
Bei hizo ziliathiriwa na janga la corona na vita vinavyoshuhudiwa katika nchi mbalimbali.
Bw Munya alisema wakulima sasa wataweza kupata mbolea kwa bei hizo mpya katika maduka yote ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB). Mashirika haya ya serikali yatauza mbolea hizo kwa bei nafuu iliyokubaliwa.
Kadhalika, Bw Munya aliwataka wakulima wote watumie fursa hiyo ili kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.
“Msimu wa mvua umeanza. Wakulima wengi wameanza kuandaa mashamba yao kwa ajili ya kupanda. Kwa hivyo ninahimiza kila mkulima kuchukua fursa hiyo na kununua mbolea ifaayo,” akasema Bw Munya.
Kwa upande mwingine, alisema kuwa wakulima watapunguziwa gharama ya kusafiri hasa wakati wanapoenda kununua mbolea kutoka kwa NCPB.
“Wakulima pia watapunguziwa gharama ya usafiri kwa Sh200.”
Wakulima wanaruhusiwa kununua tu hadi magunia 10 ya mbolea ambayo yanajumuisha mifuko mitano ya mbolea ya kupandia na mifuko mingine mitano ya mbolea ya kukuza ukuaji.
Kwa sasa, bei ya fataliza aina ya DAP itauzwa Sh2,800 kutoka kwa Sh6,000.
Bei ya mbolea aina ya CAN itakuwa Sh1,950, UREA itakuwa Sh2,700, NPK itakuwa Sh3,000, MOP itaizwa Sh2,500 huku mbolea ya Sulphate of Ammonia kuuzwa Sh2,500.