KATIKA shamba lenye ukubwa wa nusu ya robo ya ekari, kijana mmoja anachuma hela kwa kuendeleza ufugaji.
Huwafuga kuku, bata na mabatabukini, mbuzi, sili, na sungura.
Mkulima huyo ametambuliwa na rais Uhuru Kenyatta kwa juhudi zake za kilimo, mbali na kutambuliwa na mashirika yasiyokuwa ya serikali.
Kevin Uduny pia ni mwenyekiti wa kikundi cha Huruma Town Youth Group, kinachoendesha shughuli zake katika mtaa wa Huruma.
Alianzisha kikundi hicho na wengine wanne zaidi ya miaka kumi iliyopita, kama njia ya kujiajiri na kujinasua kutoka kwa ulimbo wa umaskini.
Mkulima huyu anasema kuwa, ugumu wa maisha na changamoto za mtaani zilichangia kujitosa kwa shughuli za ufugaji.
“Tunajilisha na tunataka kuhamasisha jamii ili vijana wakue. Lakini ni lazima tujilishe kwanza,” asema mkulima huyo.
“Nilianza kufanya shughuli za ukulima nikiwa mtoto mdogo kabla mamangu hajafa. Alikuwa ameniambia kitu kimoja; kuwa katika siku za usoni, ningekuwa mkulima mkubwa. Kwa hivyo, ninaamini hiyo ni baraka,” asema Uduny.
Mkulima huyo ana zaidi ya kuku 300, na huuza trei moja ya mayai kwa Sh500.
“Tukichinja mbuzi, huwapa watu nyama,” aongeza.
Yeye huwafuga kuku wa kienyeji na hukusanya mayai zaidi ya 100 kwa siku moja kutoka kwa kuku wanaotaga.
Aidha, huuza kuku hao kwa bei tofauti tofauti, kwa kutegemea jinsia, umri, uzani, miongoni mwa mambo kadhaa yanayozingatiwa wakati wanapouzwa.
“Siwezi kuwaridhisha wateja sokoni. Ninatumia sehemu ndogo, ambayo pia ni changamoto. Hatuwezi kumtosheleza kila mtu kwa sehemu hii ndogo,” adokeza Uduny.
Alianza kuwafuga kuku mnamo mwaka 2014.
Vibanda ambavyo yeye huvitumia kuwafuga kuku vimejengwa kwa mbao na mabati.
Mkulima huyo, pamoja na wenzake, walipata ufadhili kutoka kwa mradi wa serikali alipokuwa akianzisha shughuli za ufugaji.
Mwanachama wa Huruma Town Youth Group akiwalisha kuku na ndege wengine. PETER CHANGTOEK
Hii ilikuwa ni mbinu ya serikali kujaribu kupunguza umaskini katika mitaa ya mabanda.
“Nilipata ufadhili wa Sh150,000 kutoka kwa serikali; pesa ambazo nilitumia kuanzisha shughuli za kilimo,” afichua mkulima huyo, akiongeza kwamba ufadhili huo ulitolewa kupitia kwa mradi wa Njaa Marufuku.
Akaanzisha mradi wa ufugaji wa mbuzi wa maziwa. Hata hivyo, baada ya miaka kadhaa, akaanzisha shughuli ya ufugaji wa kuku, sungura, sili na ndege kadhaa.
Ana mbuzi kadha wa kadha wa maziwa, anaowauza kwa Sh8,000-Sh25,000.
Hutumia lishe za hay pamoja na zile anazozinunua kutoka kwa maduka ya kuuza lishe za mifugo.
Mbali na kuwafuga kuku na mbuzi wa maziwa, mkulima huyo pia, huwafuga sungura na sili.
Ana sungura kadhaa, ambao huwauza kwa bei tofauti tofauti.Uduny huwafuga sungura aina tofauti, mathalan; Californian White, New Zealand White na Chinchilla.
Huwauza sungura hao kwa Sh800-Sh1,500.
Bei za sungura hutegemea jinsia yao, umri na uzani wao.
Vilevile, huwafuga wanyama aina ya sili, wanaojulikana kwa Kiingereza kama guinea pigs.
Wanyama hao hufanana sana na sungura, na ni vigumu mno kwa mja kuwatofautisha na sungura. Hata hivyo, wao ni wadogo kiasi, ikilinganishwa na sungura.
Wanyama hao, aghalabu hutumika katika maabara mbalimbali wakati wa majaribio ya kisayansi na kimatibabu.
Anasema kuwa katika siku za usoni, anapania kulinunua shamba litakalomwezesha kuzipanua shughuli za kilimo, na kumwezesha kuwapa ajira vijana wasiokuwa na ajira mtaani.
“Mipango yangu ya siku zijazo ni kumiliki shamba ili kuniwezesha kufanya kilimo zaidi na kufanya uchakataji na hivyo kuongeza mapato,” asema mkulima huyo.