Algeria pazuri kufuzu kwa Kombe la Dunia baada ya kulaza Cameroon jijini Douala
Na MASHIRIKA
MABINGWA wa Kombe la Afrika (AFCON) 2019, Algeria, waliweka hai matumaini ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka huu baada ya kupokeza Cameroon kichapo cha 1-0 ugenini mnamo Ijumaa usiku katika mkondo wa kwanza wa mchujo wa mwisho.
Wakichezea jijini Douala ambako Cameroon hawakuwa wamewahi kupigwa tangu mwaka wa 2000 katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za AFCON, Algeria walifungiwa bao la pekee na la ushindi kupitia kwa fowadi veterani Islam Slimani. Bao hilo lilikuwa zawadi tosha kwa kocha wa Algeria, Djamel Belmadi aliyekuwa akiadhimisha miaka 46 ya kuzaliwa.
Slimani ambaye ni fowadi wa zamani wa Leicester City, alipachika wavuni goli la Algeria katika dakika ya 40 baada ya kushirikiana vilivyo na Youcef Belaili na kumwacha hoi kipa matata wa Ajax, Andre Onana.
Algeria almaarufu The Desert Foxes wanapigania fursa ya kunogesha fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya tano na watarudiana na Cameroon jijini Algiers mnamo Machi 29, 2022. Cameroon ndio wanaojivunia rekodi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mara nyingi zaidi (mara saba) miongoni mwa mataifa yote ya bara Afrika.
Algeria walishuhudia rekodi yao ya kutoshindwa katika mechi 35 mfululizo ikifikia kikomo nchini Cameroon mnamo Januari 2022 wakati wa fainali za AFCON zilizotamalakiwa na Senegal wanaoorodheshwa wa kwanza barani Afrika.
Mnamo Ijumaa, jumla ya mashabiki 50,000 walijitokeza kushabikia Cameroon katika uwanja wa Japoma ambapo Algeria walipotezea mechi mbili na kuambulia sare mara moja wakati wa makala ya 33 ya fainali zilizopita za AFCON.
“Hatutishwi na rekodi mbovu ya awali ya Algeria ugani Japoma. Lengo letu ni ushindi na tuna matumaini tele,” akasema fowadi wa Manchester City, Riyad Mahrez alipoongoza kikosi chake cha Algeria kutua nchini Cameroon.
Kocha Belmadi alikumbatia mfumo wa 5-2-3 kwa mara ya kwanza tangu aaminiwe mikoba ya Algeria mnamo 2018.
Cameroon walianza mchuano kwa matao ya juu huku fowadi wao anayechezea Olympique Lyon ya Ufaransa, Karl Toko Ekambi akimshughulisha vilivyo kipa wa Algeria, Rais M’Bolhi.
Kinachowaaminisha zaidi Algeria wanapojiandaa kwa marudiano ni kwamba hawajawahi kupoteza mchuano wowote kati ya 40 iliyopita ugani Mustapha Tchaker tangu waanze kuutumia mnamo 2004. Uga huo ndio utakaotumiwa kwa ajili ya mchuano wa mkondo wa pili dhidi ya Cameroon.
Mshindi kati ya Algeria na Cameroon baada ya mechi za mikondo miwili atakuwa miongoni mwa timu tano zitakazowakilisha bara la Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia mnamo Novemba-Disemba 2022 nchini Qatar.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO
Next article
TUSIJE TUKASAHAU: Mikakati ya serikali kukabiliana na baa…