MMILIKI wa kampuni ya biashara ya utalii Tom Oywa Mboya alipatikana na hatia ya kujariibu kumuua mmiliki wa hoteli ya Ronalo almaarufu Kosewe , William Osewe.
Hakimu mkuu Martha Mutuku alimpata Mboya kwa hatia ya kujaribu kumuua Osewe.Mahakama ilisema Mboya alikuwa amelaumiwa na Osewe kwa kumkonyezea jicho mkewe.
“Mlalamishi alikuwa akidai Mboya alikuwa analala na mkewe na ndio maana alijaribu kumuua,” alisema Bi Mutuku.Siku ya kujitetea , Mboya alieleza mahakama alimpiga risasi Osewe mara nne akidai “ni mnyama”
Kutokana na matamshi hayo , hakimu alimsukuma mshtakiwa jela siku moja apate adabu ya kuheshimu binadamu wenzake.Akisoma mukhutasari wa ushahidi, Bi Mutuku alisema upande wa mashtaka ulithibitisha mshtakiwa alimpiga Osewe risasi kwa lengo la kumuua.
Bi Mutuku alimpata na hatia Mboya baada ya kutupilia mbali ombi la mshtakiwa la kutaka apewe nafasi awaite mashahidi wanne kabla ya hukumu kupitishwa.Huenda Mboya akasukumwa jela kifungo cha maisha gerezani kwa kujaribu kumuua Bw Osewe , anayemiliki hoteli ya K’Osewe iliyoko kati kati mwa jiji la Nairobi maarufu kwa kuandaa samaki.
William Osewe aliyepigwa risasi…PICHA/RICHARD MUNGUTI
Ushahidi uliowasilishwa korti ulibaini mshtakiwa alimtwaga Bw Osewe risasi kwa sababu ya mwanamke.Ombi hili Bw Mboya kupitia kwa wakili Benjamin Makokha lilishangaza kiongozi wa mashtaka Bw Anderson Gikunda aliyesema “hii ni mbinu ya kuchelewesha haki ikitendeka.”
Bw Gikunda aliomba korti itupilie mbali ombi hilo la mshtakiwa akisema “alibadilisha fikra baada ya kuona ushahidi uliotolewa dhidi yake umethibitisha alikuwa na nia ya kumuua Osewe.”
Bw Makokha anayemtetea mshtakiwa huyu pamoja na wakili mwenye tajriba ya juu Profesa Tom Ojienda aliomba mahakama imruhusu mshtakiwa awasilishe ushahidi aliosema “utasaidia mahakama kufikia uamuzi wa haki.”
Bw Makokha alisema mshtakiwa haogopi kusomewa hukumu lakini akaomba korti izingatie maamuzi ya hapo awali ambapo upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi zaidi hata baada ya kufunga kesi.
Mahakama itatoa uamuzi Septemba 27, 2021 ikiwa itamruhusu mshtakiwa kuwasilisha ushahidi zaidi ama itasoma uamuzi wake.Bw Mboya amekanusha shtaka la kujaribu kumuua Osewe katika mtaa wa Garden Estate.