Baadhi ya Wazee wa Kaya waunga Sonko Mombasa
NA FARHIYA HUSSEIN
BAADHI ya wazee wa Mijikenda wameunga mkono azma ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko kugombea ugavana kaunti ya Mombasa.
Wakizungumza mjini Mombasa wakiongozwa na Bw Mwinyi Mwalimu wazee hao walikaribisha uamuzi wa Bw Sonko kujiunga na kinyang’anyiro cha ugavana Mombasa.
“Tuna furaha Bw Sonko amejiunga na siasa za Mombasa. Tumeona maendeleo yake huko Nairobi na ni wakati wetu sasa. Viongozi tuliowachagua hapo awali wametusahau sana,” akasema Bw Mwinyi.
Bw Mwinyi anaongeza kuwa wanasiasa hao hutafuta kura kutoka kwao pekee na wakichaguliwa hawaonekani mashinani wakiingia ofisini.
“Tunaamini Bw Sonko ndiye ataleta mabadiliko tunayohitaji, tuna imani naye. Wanaopinga azma yake ya kugombea wanaogopa tu uongozi wake,” alisema.
Wazee hao walisema kwamba wanahisi kutengwa kwa miaka mingi.
“Watu wanapata hofu kwa sababu Bw Sonko ni mtu wa msimamo wake,” akasema Bw Mwinyi.
Walikashifu wanaopinga ombi la Bw Sonko wakisema wanaeneza propaganda.
“Yeye (Sonko) alifanya kazi nzuri Nairobi. Alikuwa muwazi na msema ukweli na hilo ndilo lililowafanya watu wamuogope hadi wakamtupa nje ya serikali. Tunamkaribisha alete mabadiliko sawa Mombasa. Ni wakati wetu,” akaongeza Bw Mwinyi.
Mzee mwingine, Bw Ali Bege alisema Wakenya hawafai kufuata uongozi wa ukabila.
“Watu wanasema Bw Sonko si mkazi wa Mombasa. Lakini katiba yetu inaruhusu mtu yeyote kugombea nyadhifa wowote katika sehemu yoyote ya nchi hii ikizingatiwa kuwa yeye ni Mkenya,” akasema Bw Bege, akibainisha kuwa jamii ya Mijikenda ndiyo chimbuko la watu wa pwani.
Aliwataka waaazi wa Mombasa kutobagua na kutoa nafasi kwa wote.
“Sisi watu wa Mombasa tumekuwa tukikumbwa na tatizo sugu la taka kwa miongo kadhaa. Lakini Bw Sonko juzi alisafisha sehemu, ikiwa atachaguliwa kutakuwa na mabadiliko Mombasa,” akasema Bw Bege.
Wakati huo huo Bw Sonko ameonya Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ikome kuzungumzia kesi kuhusu magavana waliotimuliwa mamlakani na iache korti iamue kuhusu suala hilo tata.
Bw Sonko ambaye analenga kuwania kiti cha ugavana wa Mombasa kupitia tikiti ya Wiper, amemtaka DPP Noordin Haji ajizuie kujihusisha na siasa na amakinikie kazi yake.
Anadai kuwa Bw Haji analenga kushawishi Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) kuamua wanasiasa ambao wataidhinisha kuwania vyeo vya kisiasa.
“Awache korti ziamue kwa sababu hahusiki na hili suala. Analenga kunikera na taarifa aliyotoa ambayo inapendelea baadhi ya wawaniaji ambao ni wapinzani wangu,” akasema Bw Sonko.
“Najua umetumwa na marafiki zako kutoka Mombasa uzime ndoto zangu na kunisawiri kama mtu ambaye hatakikani lakini fahamu kuwa hakuna mtu aliye zaidi ya Mwenyezi Mungu,” akaongeza.
Bw Sonko alikuwa akimjibu Bw Haji ambaye alitoa taarifa kuwa wale ambao maadili yao yana doa hawataruhusiwa kuwania cheo chochote cha kisiasa.
Next article
Nitakuwa na mshauri maalum wa masuala ya wanawake, Nassir…