– Wabunge kadhaa wanazidi kulipa gharama ya kuwa wafuasi sugu wa DP Ruto na siasa zake za Ikulu 2022
– Ngirici amekuwa wa hivi maajuzi kuangukiwa na shoka kali ambalo limeelekezwa kwa wanaoegemea upande wa DP
– Alitimuliwa kutoka kamati ya bunge kuhusu fedha Jumatano, Julai 15 lakini akasema anajivunia kazi aliyochapa
Mwakilishi wa kina mama kaunti ya Kirinyaga Wangui Ngirici ametimuliwa kutoka kamati ya bunge kuhusu fehda na mipangalio.
Ngirici aliangukiwa na bakora ya Rais Uhuru Kenyatta Jumatano, Julai 15 katika vita ndani ya chama cha Jubilee kuwalenga wandani wa Naibu Rais William Ruto.
mwakilishi wa kina mama kaunti ya Kirinyaga Wangui Ngirici. Ngirici alitimuliwa kutoka kamati ya bunge Jumatano Julai 15. Source: Facebook
Kupitia kwa mtandao wake wa Twitter, Ngirici alisema anajivunia wakati aliohudumu kwenye kamati hiyo.
“Imekuwa ni fahari yangu kuhudumu katika kamati hiyo. Asanteni nyote mlioniunga mkono. Leo naondoka nikijivunia kazi niliyowafanyia Wakenya,” alisema Ngirici.
Ngirici ni mmoja wa wandani wa Naibu Rais William Ruto na kubanduliwa kwake kutoka kamati hiyo kunaonekana kuwa mjeledi kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta.
Kenyatta amekuwa akiongoza Jubilee kuwatimua wote wanaoshikilia nyadhifa na ni wafuasi sugu wa DP Ruto.
Ngirici amekuwa mwanaTangatanga mashuhuri na sauti yake imekuwa wazi ndani ya kundi la Inua Mama ambalo lilikuwa likimpigia debe DP kabla ya janga la Covid-19 kubisha.