Utalii: Balala awataka wawekezaji kusaka soko jipya
NA WINNIE ATIENO
Waziri wa Utalii Najib Balala amewataka wawekezaji wa sekta hiyo kusaka soko katika mataifa ya kigeni ili kufufua utalii wa kimataifa iliyodorora kufuatia janga la corona.
Akiongea kwenye mahojiano na runinga ya KTN, Bw Balala alisema baada ya janga la corona, sekta hiyo ya kimataifa ilizorota lakini serikali imebuni mbinu mpya ya kuvutia watalii.
“Tunauza Kenya ulimwenguni ili watalii wa kimataifa waje. Kadhalika, tunasaka soko la humu nchini na lile la kitaifa. Marekani, Uingereza, Ujjerumani na Uropa imekuwa soko letu la kawaida lakini sasa tunapania Saudi Arabia na China,” alisema Bw Balala.
Alisema wizara yake inaanza kuvutia watalii wa kimataifa hasa wale matajiri akisema Kenya imetunukiwa vivutio vya watalii ikiwemo wanyama pori huko Masai Mara na msafara wa Nyangumi huko Watamu. Bw Balala alisema spoti kama mbio za magari na gofu ni kivutio vya utalii.
“Lazima tutumie vivutio vyetu vya utalii kuvutia watalii wengi zaidi. Kuna watu ambao wanataka kuja Kenya kuangalia ndege zetu misituni, lakini ni sharti tuhifadhi mazingira yetu. Pia lazima tukumbatie teknolojia kusaka watalii,” alisema Bw Balala.
Alisema mabalozi wa utalii akiwemo mwanamitindo Naomi Campbell na mkimbiaji Eliud Kipchoge wanauza Kenya ulimwenguni.
Bw Balala alisema 2019 ilikuwa mwaka bora zaidi kwa utalii ambapo watalii milioni moja waliingia humu nchini. Lakini Mwaka 2021 wageni walisalia 900,000.
“Sekta yetu itaimarika na kuipiku ile mwaka wa 2019 sababu watalii wa humu nchini wameipika jeki utalii, lakini tunataka soko la kimataifa pia lirejee na kuna matumaini sababu ya uwekezaji wa serikali katika miundo mbingu hasa barabara ya mwendokasi ambayo itasaidia uchukuzi wa jiji la Nairobi,” alisema.
Haya yanajiri siku chache baada ya wadau wa sekta ya Utalii eneo la pwani kutoa wito kwa serikali kuruhusu ndege za kimataifa kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi huko Mombasa bila kupitia Nairobi.
Walitaka serikali kutoa vibali kwa kampuni za ndege kutua Mombasa.
Wakizungumza eneo la Mombasa ambapo walikuwa na mkutano na wakuu wa Fly Emirates, wadau wa vyama tofauti vya watalii waliitaka serikali kushughulikia suala hilo.
“Utalii umekuwa ukididimia sababu ya ndege za kimataifa kunyimwa vibali kutua Mombasa. Tumekutaka na mashirika tofauti ya ndege ambayo yanataka kusafiri moja kwa moja hadi Mombasa,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Utalii wa Pwani Nchini (KCTA), Bw Victor Shitakha.
Sekta ya Utalii imeajiri watu 50,000 katika ukanda wa pwani.
Bw Shitakha aliisihi serikali kupanua viwanja vya ndege vya Diani na Malindi ili kukuza utalii wa kimataifa.