PHILEMON Etyang almaarufu Baraka Phil alizaliwa akiwa na tatizo la kutosikia vizuri.
Alipozidi kukua, baadhi ya jamaa na marafiki ambao hawakuifahamu hali yake wangemdhulumu na kumwadhibu kimakosa. Walimchukulia kuwa mjeuri aliyepuuza kila wito kimakusudi. Wengine walimtenga!
Katika juhudi za kujitambua na kujisaka upya, alihiari kujiliwaza kupitia nyimbo. Aliimba sana akiwachunga mifugo wao malishoni. Shule ilimpa fursa nyingi za kuwa ngoi katika mashindano ya ngazi na viwango tofauti. Wazazi nao walimruhusu ajiunge na makundi ya uimbaji na uigizaji yaliyokuwa yakitumbuiza waumini kanisani.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa safari ya Baraka Phil katika uimbaji wa nyimbo za Injili. Alitamba kirahisi kutokana na ukakamavu, umilisi wa Kiswahili na kipawa cha ulimi kilichomfanya wembe katika ulumbi. Alijizolea tuzo za haiba kutoka kwa walimu na umaarufu ukaanza kumwandama akiwa mwanafunzi wa darasa la nane.
Tangu wakati huo, hakupoteza dira wala kurudi nyuma kisanaa. Ari yake ya kuimba ilichochewa zaidi na mwanamuziki Alex ‘Ringtone’ Apoko aliyeizuru shule yao ya upili mnamo 2009 na kuwahimiza wajitahidi kufikia upeo wa ndoto zao.
Baraka Phil alishiriki tamasha za muziki na akaongoza shule yake ya upili ya Kolanya Boys iliyoko Kaunti ya Busia kufika kiwango cha kitaifa jijini Mombasa mnamo 2009. Alijikuza zaidi kisanaa akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), Bewa la Taita Taveta. Alijiunga na Jumuiya ya Mtakatifu Rita, akawa mwimbaji wa tenzi kanisani.
Philemon Etyang Mamai almaarufu Baraka Phil wakati wa mahojiano. PICHA | CHRIS ADUNGO
Mnamo Februari 2020, Baraka Phil alikutana na prodyusa Shallz Baro aliyemsaidia kurekodi wimbo ‘Na Wonder’ uliofyatuliwa rasmi Novemba 2021 chini ya mwavuli wa Alchemy Musiq Studios. Kibao hicho kilimchochea kutoa wimbo ‘Nguvu ya Yesu’ mnamo Februari 2022.
Mbali na nyimbo ‘Ni Salama’ na ‘Alakara’ alizozitoa katika mwaka wa 2021, kibao kingine kilichomkweza Baraka Phil kimuziki na kumzolea sifa sufufu ulingoni ni ‘Papa’ alichokiachilia Julai 2020 kupitia Kembo Music Studios.
Kubwa zaidi katika maazimio yake kisanaa ni kuchomoa wimbo kila baada ya miezi miwili na kutoa albamu baadaye mwaka huu. Anapania pia kushirikiana na wanamuziki Florence Andenyi, Ali Mukhwana, Timothy Kitui, Tumaini Akilimali na Walter Chilambo kutumia uimbaji kueneza Ukristo, kukuza maadili na kuipa jamii mwelekeo.
Baraka Phil alilelewa katika kijiji cha Kabkara, eneobunge la Sirisia, Kaunti ya Bungoma. Ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto saba wa Bi Maclean Echakara na marehemu Bw Joseph Mamai.
Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Machakha, Sirisia (2000-2007) kabla ya kujiunga na Kolanya Boys, Teso Kaskazini (2008-2011). Japo matamanio yake ya tangu utotoni yalikuwa kuwa rubani, alisomea masuala ya usimamizi wa ununuzi na ugavi chuoni JKUAT (2012-2016). Amekuwa akisimamia shughuli za usambazaji wa bidhaa za kampuni moja jijini Nairobi tangu 2017.
Anashikilia kuwa siri ya kufaulu katika tasnia ya muziki ni kumtanguliza Mungu, kuwa na stahamala, kujituma na kujiamini.
“Fahamu unachokitaka na utambue unakokwenda. Jifunze kujikubali na usijihukumu wala kutamauka changamoto zinapobisha,” anashauri.