Bulls wakunjwa pembe mduara nusu na 360 Media kocha wao akilalamikia safu ya ulinzi
Na PATRICK KILAVUKA
Kocha wa Young Bulls Issa Wistone alikariri kwamba safu ya ulinzi ilionesha utepetevu kwa kiasi hali ambayo ilisababisha 360 Media ikikunja pembe mduara nusu kwa kuandikisha sare ya 2-2 katika mchuano wa kusaka alama za Ligi ya Kitaifa Daraja ya Pili, uwanjani Kihumbuini, Jumapili.
Aidha, kocha wa 360 Jerey Opondo naye aliwapongeza vijana kwa kuonyesha mchezo safi ugenini licha ya kipa kulegea kidogo na kufanya wapinzani kufuta goli la pili mbali na kutatizika kuchezea uwanja huo. Wafungaji wa Bulls walikuwa Benito Kambele dakika ya 11 na Evans Miriti dakika ya 75 ilhali Media walipachikwa na Bonface Ontere dakika ya 32 na Adams Nyambane dakika ya 66.
Young Bulls jezi ya kijani kibichi wakichuana na 360 Media uwanjanI Kihumbuini…Picha/PATRICK KILAVUKA
Kwingineko, katika mchuano wa Kaunti-ndogo FKF, Nairobi West ambao uliandaliwa uga wa AHITI, Unfit FC waliwakomoa Starehe Sports Club 3-1. Magoli ya Unfit yalititigwa na Rajab Omari dakika ya 25 na Wafula B (mawili) dakika ya 65 na 80 ilhali Starehe walifuta machozi kunako dakika ya 53 kupitia tuta la Junior D.
Marefa wakiongozwa na Harry Murito ambao walichezesha mechi ya Young Bulls na 360 Media wakiongea na makapteni wake zote…Picha/PATRICK KILAVUKA