[ad_1]
Chelsea, Real Madrid vitani Uefa
NA MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
CHELSEA walichapwa 4-1 na Brentford ligini ugani Stamford Bridge mwishoni mwa wiki, lakini matokeo hayo yanatarajiwa kuwekwa kando watakaporejea uwanjani humo kuvaana na Real Madrid katika pambano la robo-fainali ya UEFA mkondo wa kwanza, leo Jumatano usiku.
Kichapo hicho kilikuwa cha kwanza katika mechi sita katika mashindano makubwa tofauti tangu washindwe na Liverpool kwenye fainali ya Carabao Cup kupitia kwa mikwaju ya penalti, kichapo hicho kikiwa cha tano tu katika muda wa kawaida tangu msimu huu uanze.
Baada ya kushindwa 5-2 na West Ham United, Chelsea walijirekebisha na kuichapa FC Porto 1-0 katika mkondo wa kwanza wa mechi za Klabu Bingwa na kufuzu kwa raundi ya 16 Bora.
Baadaye waliibuka na ushindi wa jumla wa 4-1 dhidi ya Lille katika hatua ya 16-Bora.
Kwa upande mwingine, Real Madrid watakuwa wakitafuta kulipiza kisasi baada ya Chelsea kuvuruga juhudi zao walipowabandua katika nusu-fainali msimu uliopita.
Kikosi hicho cha kocha Carlos Ancelotti kilikaribia kuondolewa katika hatua ya 16-Bora baada ya kuchapwa 2-0 na Paris Saint-Germain (PSG) katika mkondo wa kwanza, kabla ya nahodha Karim Benzema kufunga mabao matatu katika mkondo wa pili na kuisaidia timu hiyo kusonga mbele.
Lakini mambo sio mazuri sana kwa kikosi hicho baada ya majuzi kuchapwa 4-0 na Barcelona ugani Santiago Bernabeu, ingawa wikendi walijitahidi na kuibuka na ushindi finyu wa 2-1 dhidi ya Celta Vigo kwenye pambano la Ligi Kuu ya La Liga.
Chelsea wanatarajiwa kumtegemea Christian Pulisic kuongoza safu ya mashambulizi baada ya Mwaamerika huyo kufunga mabao sita katika mechi za awali katika mashindano haya, mbali na kutoa pasi zilizochangia kupatikana kwa mabao.
Licha ya majuzi kushindwa na Brentford, Chelsea chini ya kocha Thomas Tuchel wamekuwa na historia nzuri katika mashindano ya Klabu Bingwa.
Next article
KCPE 2021: Changamoto tele Mukuru hazikuzima bidii yao…
[ad_2]
Source link