Katika ripoti ya The Standard, wabunge 20 wanaripotiwa kufanyiwa vipimo baada ya kutagusana na afisa mkuu wa Bunge la Kitaifa ambaye kwa sasa amelazwa.
Mbunge huyo ambaye amelazwa katika chumba cha watu mahututi anasemekana kutangamana na wenzake wawili ambao wamelazwa, Mbunge wa mara ya kwanza kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya na mwingine wa Pwani.
“Hii ni tishio kubwa. Wengi wao ambao walitangamana naye wamelazimika kwenda kupimwa, na hii idadi yaweza kupanda kufikia Jumatatu wakati matokeo ya wengi wao ambao walipimwa yatatolewa.
“Ninajua yamkini wabunge sita wamepatwa na virusi na wako hospitalini, mmoja yuko ICU,” alifichua mbunge mmoja ambaye jina lake lilibanwa.
Karani wa Bunge la Kitaifa Michale Sialai, alisema uongozi wa Bunge hauna habari yoyote ya endapo wanachama wake wanaugua COVID-19 na kushikilia kwamba masuala ya afya ni jambo la faragha na huanikwa hadharani endapo wagonjwa wameidhinisha kutolewa kwa taarifa hiyo.
Sialai alisema viongozi wanaweza kuwa hawana taarifa kuhusu wabunge ambao walipatwa na virusi kwa sababu hali ya afya ya wabunge ni masuala ya faragha lakini inawahusu wabunge wengine ambao wanataka kuzingatia mikakati ya usalama.
“Endapo ni kweli basi ni suala la kutiliwa maanani lakini kwa sasa hakuna ripoti iliyowasilishwa kwetu kuhusu kisa chochote,” alisema Sialai.
Karani wa Bunge la Kitaifa Michale Sialai, alisema uongozi wa Bunge hauna habari yoyote ya endapo wanachama wake wanaugua COVID-19. Picha: Capital FM. Source: UGC
Japo Sialai alisema viongozi wa Bunge la Kitaifa wako makini kuwaweka Wabunge salama, wanaweza kufanya hivyo tu kulingana na masharti ya bunge.
Ripoti hiyo inakujia kufuatia ghadhabu kutoka kwa umma dhidi ya Wabunge kukiuka sheria za COVID-19 katika hafla kadhaa za siasa huku picha zikiibuka wakiandaa hafla za hadhara bila kuzingatia sheria ya kukaa mbali.
Ikulu pia ilimulikwa hivi majuzi baada ya wafanyakazi wanne kugunduliwa kuwa na virusi hivyo.