MAKALA MAALUM: Dalili fiche za kuvu, maradhi hatari kwenye kucha zako
WANGU KANURI NA LEONARD ONYANGO
CHARITY Kariuki alipoona ukucha wake wa kidole gumba una madoadoa meupe, alidhani ilikuwa kawaida tu.
Alianza kuingiwa na wasiwasi ngozi inayoshikana na kucha ilipoanza kutoa usaha na kuwa nyeusi.
Alipoenda hospitalini daktari alimweleza kuwa alijiumiza wakati wa kukata ukucha huo.
“Nilipewa dawa lakini hakukuwa na mabadiliko hata baada ya kumaliza tembe alizonipa. Ukucha ulibadilika kuwa mweusi,” anaeleza.
Bi Kariuki, 24, alirudi hospitalini kufanyiwa upasuaji na ukucha huo ukang’olewa.
“Baada ya kung’olewa ukucha nilikuwa nadungwa sindano mara mbili kwa siku kwa wiki tatu,” anasema.
Ukucha mwingine ulimea lakini ukasalia kuwa mweusi – hali iliyompa wasiwasi zaidi.
Lakini kilichomshtua zaidi madoadoa yalitokea kwenye kidole gumba cha mkono mwingine wa kushoto.
Madoadoa hayo yalisambaa kwenye vidole vingine vya mikono yote. Mtaalamu wa magonjwa ya ngozi baadaye alimweleza kuwa alikuwa akihangaishwa na maambukizi ya kuvu (fungal infection).
Kulingana na Dkt Hashim Kaderbhai, mtalaamu wa ngozi katika hospitali ya M.P. Shah, yeye hutibu idadi kubwa ya watu walioota kuvu katika kucha zao kila mwezi.
“Maambukizi ya kuvu kwenye kucha huwa ya aina tofauti. Mtu hujua ana ugonjwa wa kuvu kwa kucha (onychomycosis) wakati kucha zinakuwa za rangi ya manjano, kahawia au nyeupe kisha kuwa nyeusi.”
Anasema kuwa ugonjwa wa onychomycosis huathiri watu ambao hutangamana na maji sana na wale ambao hurembesha kucha kwa kutumia rangi ya kucha (gels).
“Watu wanaosha vyombo, wanaofua nguo, na wanaoongeza urefu wa kucha zao kwa kubandika kucha bandia wanajitia katika hatari ya kupata onychomycosis kwani wanasaidia kuvu ‘kumea’ na kuenea kuchani.”
Dkt Kaderbhai anaonya kuwa wagonjwa wa kuvu wanaojitibu bila ushauri wa madaktari wanajiongezea matatizo badala ya kujisaidia.
Matibabu ya kuvu yanaweza kuchukua kati ya mwezi mmoja hadi zaidi ya miezi sita kabla ya mwathiriwa kupata nafuu.
Dkt Kaderbhai anasema kuwa ugonjwa wa kuvu unaweza kusambazwa kwa wanafamilia iwapo mmoja wao anaugua maradhi hayo.
“Onychomycosis huenea maeneo yenye unyevunyevu kama mabwawa ya kuogelea, vyumba vya mazoezi na kabati za kuweka mavazi ya wanaspoti.”
Watu waliozeeka pia hupata ugonjwa wa kuvu sana ikilinganishwa na vijana sababu baada ya migongo yao kupinda, wao hutatizika kuweka kucha zao zikiwa safi na kufanya kuvu kumea.
Kutokahikisha kuwa viatu unavyovaa ni safi husaidia kuvu kukua kwani Wakenya wengi huvalia viatu vyao kwa muda wa zaidi ya saa nane.
“Matibabu ya kuvu bila mgonjwa kudumisha usafi wa viatu vyake ni kazi bure kwani viini vya onychomycosis vitaendelea kuwepo,” anasema.
Dkt Kaderbhai anaonya kuwa kupaka kucha rangi (cutex) hakusaidii kuzuia ugonjwa wa kuvu.
“Madai kwamba rangi ya cutex inazuia kuvu kuathiri kucha ni potovu na hayafai. Ushauri wa aina hiyo amba0 mara nyingi hupatikana mitandaoni haufai,” anaelezea.
Wataalamu wanasema kuwa watu walio na matatizo ya kiafya haswa yanayofanya kinga ya mwili kufifia wako katika hatari kubwa ya kukabiliwa na kuvu.
Watu waliofanyiwa upasuaji au waliopata jeraha kwenye kucha, wagonjwa wa kisukari, wenye matatizo ya kusambaa kwa damu mwilini na wanariadha wako katika hatari kubwa ya kukabiliwa na kuvu, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Shirika hilo linashauri watu kuhakikisha kuwa kucha zao ni safi na kavu; kukata kucha zilizo ndefu kupita kiasi; kutotembea pasi viatu katika maeneo yenye unyevunyevu; kutotumia kifaa cha kukata kucha na watu wengine; na kuhakikisha kuwa saluni ya kucha unayozuru ni safi.
Mbali na kuvu, wataalamu wanasema kuwa kubadilika kwa rangi ya kucha kunaweza kuwa dalili ya magonjwa hatari.
Kwa mfano, Taasisi ya Kudhibiti Maradhi (CDC) inasema kuwa kucha zinapokuwa rangi nyeupe inaweza kuwa dalili ya tatizo la ini.
Kucha zikibadili rangi na kuwa manjano inaweza kuwa dalili ya ugonjwa wa kisukari au mapafu. Kucha nyeusi pia zinaweza kuwa dalili ya aina ya kansa ambayo huathiri ngozi ya chini ya kucha (subungual melanoma).
Aina hiyo ya kansa huathiri kati ya asilimia 0.07 na asilimia 2 kote duniani na wataalamu hawajui kinachosababisha ugonjwa huo.
Next article
Kizaazaa Old Trafford Man Utd ikivizia Spurs