Connect with us

General News

Dhehebu ‘jipya’ katili laendeleza ukeketaji wa watoto kisiri – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Dhehebu ‘jipya’ katili laendeleza ukeketaji wa watoto kisiri – Taifa Leo

Dhehebu ‘jipya’ katili laendeleza ukeketaji wa watoto kisiri

NICHOLAS KOMU na MERCY MWENDE

DHEHEBU moja lenye itikadi kali za kitamaduni limekuwa likiendeleza ukeketaji wa wasichana eneo la Kati mwa Kenya.

Likijulikana kwa jina Gwata Ndai, kundi hilo limekuwa likiendeleza ukeketaji kichinichini katika kaunti za Kiambu, Murang’a na Nyeri na lina makao yake katika maeneo ya Githunguri na Ndumberi, Kiambu.

Pia linahusishwa na kundi lililoharamishwa la Mungiki. Japo mwanzoni kundi hilo lilikuwa likiandaa hafla zake za kupigia debe ukeketaji kwa kisingizio cha kuendeleza mila ya jamii ya Agikuyu, lilibadili mtindo na kuanza kuendeleza tabia hiyo haramu kichinichini baada ya Askofu Mkuu Mstaafu wa Dayosisi ya Nyeri, Kadinali George Njue kuzua lalama kuhusu vitendo vyao miaka miwili iliyopita.

Kutokana na kauli za askofu huyo, polisi walizamia operesheni na kusababisha wanachama wa kundi hilo kuingia mafichoni.

Hata hivyo, Taifa Jumapili imebaini kuwa bado linaendeleza ukeketaji kwa wasichana wadogo na hata wale walio na umri wa miaka mitano pekee.

Masharti ya mwanaume kujiunga na kundi la Gwata Ndai ni kuwa lazima mkewe na watoto wa kike wapitie kisu cha ngariba.

Mara nyingi hili hutekelezwa kwa lazima ndiposa baadhi ya wanawake wamelazimika kutengana na waume wao.Vilevile Gwata Ndai inakubali waume kuwapiga wake wao na pia kuoa zaidi ya mke mmoja.

Pia wanachama wake hawataki kujihusisha na dini yoyote iwe Ukristo au Uislamu na husisitiza kuwa mgonjwa asipelekwe hospitali bali atumie dawa za kienyeji.

Mnamo Jumatatu, polisi waliwaokoa wasichana saba kutoka boma moja ambao sita kati yao walikuwa wamekeketwa katika kijiji cha Muthuthini, eneobunge la Mukurwe-Ini, Kaunti ya Nyeri.

“Tuliwatuma maafisa wetu katika boma hilo na tukapata kweli wasichana hao walikuwa wamekeketwa. Wahudumu wa afya wanaendelea kuwahudumia na wawili bado wako hospitalini,” akasema Kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Mukurweini, Patrick Manyasi.

Washukiwa saba, mmoja akiwa mwanamke, wamekamatwa pamoja na Benson Warui Muchine ambaye anaaminika kuwa kiongozi wa Gwata Ndai.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Agikuyu Wachira wa Kiago ameshutumu vitendo vinavyoendelezwa na kundi hilo eneo la Kati mwa Kenya akisema ni haramu na sio utamaduni wa jamii hiyo.