NI timu mpya iliyoundwa kwa sababu ya kusaidia wasichana wengi wa sehemu ya Ukunda kushiriki kwenye mchezo wa soka.
Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa klabu hiyo ya Diani Queens FC Michael Otieno, yeye pamoja na Kocha Fredrick Wanyonyi Wafula walionelea ni jambo la busara kuanzisha timu ambayo itawaunganisha wasichana wa tabaka mbalimbali kunoa vipaji vyao.
“Tulijionea kuwako kwa wasichana wengi waliokuwa na talanta za kucheza soka na tukawakusanya wa makabila mbalimbali na kuwaanzishia klabu ambayo imepania kuhakikisha wengi wao wanafikia viwango vya hali ya juu vya kusakata kabumbu,” amesema Otieno.
Anasema kwa wakati huu wanasaidiana na baadhi ya wahisani kwa mahitaji muhimu ya timu lakini ametoa wito kwa wahisani kujitokeza kuisaidia kwani wana nia kubwa ya kuifikisha mbali Diani Queens FC.
“Tunajisaidia sisi waanzilishi kwa hivi sasa na tumeingia kwenye ligi ya kaunti kusudi tuanze kutoka huku kwetu badala ya kukimbilia ligi ya jimbo ambayo tunataka kuingia baada ya kushinda taji,” akasema Otieno.
Afisa huyo mtendaji alimshukuru sana rafiki yake raia wa Uholanzi Sven Van Hegelsom kutoka Amsterdam kwa kuisaidia timu hiyo kwa vifaa na misaada mingine.
“Rafiki yangu huyu tutamtegemea kwa kujionea vipaji na kututafutia klabu za huko kwao,” akasema.
Otieno anasema hamu yake kubwa ni kuwaona wasichana wenye talanta wanapata fursa ya kucheza soka ya kulipwa barani Ulaya na hasa huko Uholanzi ambapo Hegelsom atafanya mipango ya kuwatuma maskauti kujionea wenyewe wachezaji wazuri.
Kocha Wafula anasema amefurahia kuwako katika timu hiyo kwani tayari kuna wanasoka ambao wameanza kuonyesha kuwa na hamu ya kucheza soka ya hali ya juu na kulenga kuwajibia timu za ng’ambo.
“Nimewafanyisha mazoezi ya kutosha na tunasubiri kwa hamu Ligi ya Kaunti ya Kwale ianze ili tuweze kuwika viwanjani. Tumejitayarisha vya kutosha na wasichana wangu wameonyesha nia ya kuhakikisha tumepata ushindi katika kila mechi tutakayocheza,” akasema Wafula.
Aliambia Taifa Jumapili kuwa kati ya mipango aliyotayarisha kwa timu hiyo ni pamoja na kuhakikisha kunapokuwa na majaribio sehemu yoyote atakuwa akiwapeleka kuwapa moyo wa kuendeleza vipaji vyao.
Baadhi ya wachezaji wa Diani Queens FC waliohudhuria majaribio ya kutafuta kikosi cha Harambee Starlets U-20 kushiriki kwenye dimba la kufuzu kwa Kombe la Dunia katika uwanja wa Mbaraki Sports Club. Picha/ Abdulrahman Sheriff
Anasema aliichukua timu nzima akaipeleka Mombasa wakati kocha wa timu ya taifa ya Harambee Starlets Charles Okere alipofika Mbaraki Sports Club kufanya majaribio ya kuchagua wachezaji wa timu ya Starlets U-20 inayoshiriki kwenye dimba la Kombe la Dunia U-23.
“Ingawa hakuna mchezaji yeyote wangu aliyefanikiwa kuchagulkiwa katika kikosi cha timu hiyo, lakini wamejifunza mengi nami nimekuwa na nafasi nzuri ya kutambua jinsi ya kuwarekebisha kwa makosa waliyofanya wakati wa majaribio hayo,” akasema mkufunzki huyo.
Timu hiyo ya Diani Queens FC imethibitisha kushiriki kwenye Ligi ya Kaunti ya Kwale na imepania kuhakikisha imeshinda taji la ligi hiyo na kupanda ngazi hadi Ligi ya jimbo la Pwani msimu utakaofuata.
“Tumejiunga na ligi hii hatukuwa na haraka ya kwenda ligi ya juu sababu tunataka kuwaunda wasichana wetu waanze ligi ya chini na kupanda ngazi hadi pale tunapoazimia kufika kwenye Ligi Kuu ya Soka la Wanawake nchini (KWFPL),” akasema Otieno.
Alisema anaamini wachezaji wake watajitahidi kuhakikisha wanafanya vizuri katika msimu wao wa kwanza kushiriki katika ligi. Klabu hiyo imeanzishwa mapema mwaka huu kwa ajili ya kuwapa fursa wasichana kuendeleza vipaji vyao.
Nahodha wa timu hiyo Ruth Kadzo amesema kwa upande wao wachezaji, wameamua kushirikiana na wakuu wa timu kuhakikisha wanaipeleka mbali timu yao hiyo.
“Tunataka tufike hadi ligi kuu ya soka ya kina dada maana kila tutakapocheza tutazidi kufanya bkidii kuhakikisha msimu unaokuja tunapanda ngazi,” akasema Ruth