Connect with us

General News

Himizo amani idumu wakati wa uchaguzi – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Himizo amani idumu wakati wa uchaguzi – Taifa Leo

Himizo amani idumu wakati wa uchaguzi

NA WAANDISHI WETU

MAELFU ya waumini wa kanisa Katoliki na Kianglikana, jana walikusanyika katika makanisa mbalimbali kusherehekea Jumapili ya Mitende huku makasisi wakiwahimiza Wakenya kuendelea kudumisha amani uchaguzi wa Agosti ukikaribia.

Baadhi yao walibeba matawi ya mtende kuashiria jinsi Yesu Kristo alivyoingia Yerusalemu kwa ushindi kabla ya kusulubishwa kwake na ufufuo uliofuata.

Jijini Nairobi, waumini katika Kanisa la Kianglikana Nchini (ACK) wakiongozwa na askofu mkuu Jackson Ole Sapit walisherehekea Jumapili ya Mitende kwa kutembelea ofisi mbalimbali za serikali zikiwemo ya Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC), mahakama, ofisi ya Rais na majengo ya bunge wakihubiri amani.

Askofu huyo alisema kuwa ofisi hizo ndizo hutegemewa sana wakati wa uchaguzi.

“Ofisi hizo nne ndizo zinategemewa sana wakati huu wa uchaguzi. Wakenya wanasubiri ukombozi mkubwa na ndio maana tukaamua kuzitembelea ofisi hizo kuhubiri amani,” akasema askofu Ole Sapit.

Kwa upande mwingine, aliwahimiza wanasiasa na Wakenya wote kuwa waangalifu na kuyachuja maneno yao wakati huu wa kampeni.

“Kila mmoja anafaa ayachuje maneno yake na kukoma kuyatumia maneno ambayo yatachochea chuki. Tuyatumie maneno yetu kuwainua watu na kudumisha amani.” Kwingineko, Padri Peter Paul Ndiema, aliwaongoza waumini katika kanisa la Sacred of Heart Cathedral, Eldoret, huku akisisitiza haja

ya wanasiasa kuvumiliana kama njia ya kuhakikisha nchi inasalia kuwa na umoja kabla na baada ya uchaguzi mkuu.

“Kila mtu atahitaji mwenzake baada ya uchaguzi na siasa zisilete mgawanyiko kati yetu. Kadiri tunavyojiunga na mirengo tofauti ya kisiasa, tuvumiliane kila wakati kama njia ya kuhakikisha tunabaki kuwa pamoja,” akasema padri Ndiema.

Katika Kaunti ya Kisumu, Padri Joseph Bekele wa parokia ya Consolata Shrine alihimiza Wakenya waendelee kuishi kwa amani ya Yesu Kristo.

“Huu ni wakati wa kuwasaidia watu wasiojiweza na kuhubiri amani. Tuepuke siasa za

chuki,” akasema padri Bekele.

Kwa upande mwingine, askofu Martin Kivuva wa Kaunti ya Mombasa, alitoa wito kwa wanasiasa waendeleze kampeni zao kwa amani na kuepuka maneno ya chuki.

“Kila mmoja achunge maneno yake wakati wa kampeni. Kila mwanasiasa ahakikishe kuwa anauza sera zake bila kuleta chuki ama kumwingilia mpinzani wake,” akasema askofu Kivuva.

Vile vile, waumini katika kaunti ya Nakuru pia walisherehekea Jumapili ya Mitende huku kila mmoja akihubiri amani.

Ripoti za Mercy Simiyu, Fred Kibor, Brian Ocharo, Eric Matara na Elizabeth Ojina