Connect with us

General News

Hospitali iliyokuwa kimbilio la wengi Kaloleni yasalia gofu – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Hospitali iliyokuwa kimbilio la wengi Kaloleni yasalia gofu – Taifa Leo

Hospitali iliyokuwa kimbilio la wengi Kaloleni yasalia gofu

MAUREEN ONGALA NA ALEX KALAMA

KWA miongo mingi iliyopita, wakazi wa Kaunti ya Kilifi na viungani mwake walijivunia sana hospitali moja ya kimishenari ambayo iliwapa huduma bora za matibabu.

Hayo yote yalitamatika ghafla, wakati hospita – li hiyo ya St Lukes Giriama iliyo Kaloleni ilipoanza kukumbwa na matatizo si haba, hadi ikasambaratika kabisa takriban miaka sita iliyopita.

Itakuwa safari ya hatua ndefu itakayochukua muda mrefu na pia kugharimu mamilioni ya pesa ili kurudisha hadhi ya hospitali hiyo. Hii ni kufatia utaratibu wa kuhakikisha kuwa vitengo vyote katika hospitali hiyo vitarejelea hali yake ya kawaida.

Subira Kwa mujibu wa Askofu Alphonse Mwaro Baya, anayesimamia Kanisa la Kianglikana la ACK jimbo la Mombasa, itabidi wananchi wawe na subra huku mikakati na taratibu za kufufua hospitali hiyo zikiendelea.

Hospitali hiyo inahitaji takribani Sh40 milioni ili kurejelea hali yake ya kawaida na kutoa huduma bora kwa maelfu wa wakaazi waliokuwa wanaitegemea. Kwa sasa hospitali hiyo iko chini ya kanisa la ACK jimbo la Mombasa baada ya kuchukuliwa kutolewa katika kitengo kinachosimamia maswala ya maendeleo katika katika la ACK (ADS) tawi la Pwani.

Iliyokuwa hospitali ya kifahari na tegemeo kwa zaidi ya wakazi 300,000 kutoka eneo bunge la Kaloleni na pia maeneo bunge jirani ya Ganze, Rabai, Kauma na Chonyi sasa imebakia kutoa huduma chache tu kwa wananchi huku majengo yakichakaa na vifaa muhimu kukosekana.

Pia kufungwa kwa shule ya kutoa mafunzo ya uuguzi ambayo ingesaidia kubuni ajira za kazi ili kumaliza umaskini katika jamii, ilikuwa ni pigo kubwa na iliua ndoto ya vijana wengi..

Hospitali ya St Lukes ilianzishwa mwaka wa 1927. Hata hivyo ilifungwa mara mbili kufuatia changamoto mbalimbali. Mara ya kwanza ilifungwa mwaka wa 2013 na serikali kwa sababu ya hali ya mbovu ya miundomsingi na usafi, hali ambayo ilihatarisha maisha ya wagonjwa na jamii.

Ilifungwa tena mwaka wa 2016 kwa sababu ya changamoto za kifedha na pia kutosajiliwa na bodi ya wahudumu wa matibabu na madaktari wa meno nchini.

Kwa sasa wakazi waliotegemea huduma bora za bei nafuu katika hospitali hiyo wanalazimika kutafuta matibabu na huduma nyingine za afya katika hospitali ya Mariakani, wengine wakiamua kwenda katika hospitali kuu ya rufaa ya kaunti ya Kilifi.

Askofu Baya alisema kuwa licha ya kuwa hospitali hiyo inahitaji Sh 40 milioni kufufuliwa, wanahitaji Sh8 milioni za dharura kutekeleza marekebisho madogo madogo ili kuanzisha tena kitengo cha kuwalaza wagonjwa.

Hata hivyo alipinga vikali pendekezo la baadhi ya viongozi kutaka kanisa hilo kutoa hospitali hiyo kwa serikali ya kaunti ya Kilifi.

“Kaunti ya Kilifi haiwezi kuchukua uongozi wa hospitali kwa sababu ni mali ya kanisa la ACK jimbo la Mombasa na hatuwezi kumpa mtu. Itakuwa safari ya hatua ndefu itakayochukua muda na kugharimu mamilioni ya pesa ili kurudisha hadhi ya hospitali hiyo yeyote,” akasema.

Katika mwaka wa 2016, Serikali ya Kaunti ya Kilifi ilitoa ufadhili wa Sh11 milioni kusaidaia katika kukarabati kitengo cha wagonjwa wanaokuja na kurudi nyumbani.

“Kaunti ya Kilifi ilitupa madaktari na wauguzi na bado tunataka kuendeleza ushirikiano huo. Pia tunataka waendelee kutekeleza majukumu mengi katika hospitali hii kadri na jinsi sheria itakavyowaruhusu,” akasema.

Aliendelea kusema shule ya kutoa mafunzo kwa waauguzi itafunguliwa tena wakati hospitali hiyo itaanza kulaza wagonjwa.

Pigo kubwa Alitaja kufungwa kwa hospitali hiyo kuwa pigo kubwa kwa jamii ambao walitegemea kituo hicho kwa matibabu.

Kwa sasa ukarabati ya wadi ya watoto imekamilika. St Lukes Giriama ilianzishwa mwaka wa 1927 na Church Missionary Society (CMS) kutoka nchini Uingereza na ikawa chini ya wamishenari hadi mwaka wa 1883 wakati kanisa la ACK jimbo la Mombasa lilopochukua uongozi wake.

Kwa sababu ya ufadhili kutoka ng’ambo kupitia Church Missionary Society, hospitali hiyo ilikuwa inatoa matibabu ya bure kwa wakazi hao.

Askofu Baya alisema kuwa hali hiyo ya kupewa matibabu ya bure imekithiri katika jamii na hawajakuwa radhi kutozwa ada zozote.

“Dhana ya kuwa huduma za afya zinatolewa bila malipo bado imekita miongoni mwa wakazi na imeathiri utendaji kazi wa hospitali hii tangu wakati wamishenari walipoondoka,”akasema.

Alizidi kusema kuwa, lengo la kanisa hilo kutoa huduma bora kwa jamii haikuzaa matunda kwani hospitali hiyo ilikuwa na deni kubwa ambalo lilikuwa limerundikana tokea wakati kanisa lilipokuwa chini ya uongozi wa CMS.

Katika mwaka wa 2020, ACK Mombasa ilisajili hospitali hiyo kama kampuni, ACK St Lukes Mission Hospital Limited. Kwa msingi huo, kampuni hiyo ina jukumu la kusimamia kufuliwa na kuendelezwa kwa hospitali hiyo.

Pia, hospitali hiyo ilibadilishwa jina na kuwa St Lukes Nursing Home. Hatua hii ilitoa nafasi kwa kuchaguliwa bodi mpya ya wakurugenzi ili kuimarisha utendakazi wa kampuni hiyo.

Wadau wamesema tofauti na awali ambapo wasimamizi wengi hawakuwa na taaluma za kiusimamizi, bodi mpya ina wasomi wa kila nyanja na wenye weledi wa maswala kusimamia sekta mbalimbali kwa hivyo kuna matumaini ya ufufuzi wa hospitali hiyo.

Tayari kanisa la ACK limechagua afisa wa afya kusimamia mipango katika hospitali hiyo na pia maswala ya dini.

Dkt Baya alisema kwa sasa wanaendeleza mazungumzo na maafisa wa kutoa huduma za bima za afya ya serikali (NHIF) katika juhudi za kuwawezesha jamii kupata matibabu kwa bei nafuu.

Changamoto sawia Hata hivyo alizidi kusema kuwa changamoto ambazo hospitali hiyo inapitia si jambo geni bali ni hali kawaida ambayo ni sawia na matatizo yanakumba hospitali zote nchini zikiwemo za kaunti, serikali kuu na pia za wamishenari.

“Changamoto ya maswala ya afya ni hali ambayo hospitali nchini zinapambambana nazo katika kila kiwango. Hospitali za kaunti zina matatizo mengi ilhali zinapata pesa nyingi kutoka katika serikali ya kitaifa. Kwangu hali hii sio geni, bali ni baadhi ya changamoto ambayo nchi yetu ya Kenya inakumbana nazo katika sekta ya afya nchini,” akasema.

Aliwatahadharisha wanasiasa dhidi ya kutumia hospitali hiyo kupiga siasa na kuwahadaa wananchi kuwapigia kura.

“Ninachojua ni kwamba hospitali hiyo inafanya kazi japo kwa kiwango kidogo, na kama kanisa tunafanya kila jitihada kuhakikisha inatoa huduma zote. Haitanichukua siku moja kuanzisha upya hospitali hiyo kwa sababu ninahitaji mamilioni ya pesa, sio milioni moja,” akasema.

“Wasione kuwa itakuwa rahisi. Washukuru juhudu zangu za kuifufua hospitali hiyo na zile hatua ambazo tumepiga,” akazidi kusema.

Hivi majuzi, baadhi ya wanasiasa katika eneo hilo waliwataka viongozi katika eneobunge la Kaloleni kushirikiana ili kutafuta njia ya kuifufua hospitali hiyo.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending