WANTO WARUI: Huenda mtihani wa mfumo wa CBC Gredi ya 6, hauna tofauti kubwa na KCPE
NA WANTO WARUI
TAASISI ya kutayarisha Mitihani nchini (KNEC) hatimaye imetoa ratiba na mwelekeo jinsi ambavyo mtihani wa Gredi ya 6 utakavyofanywa.
Katika ratiba hiyo, mtihani huo utafanywa kwa muda wa siku tatu sawasawa na ule wa KCPE.
Mtihani huo ambao unajulikana kama KPSEA (Kenya Primary School Education Assessment) utakuwa na majibu ya kuchagua kama ilivyo KCPE ila wanafunzi hawataandika insha za Kiingereza na Kiswahili.
KNEC imeamua kutumia mtihani wenye majibu ya kuchaguliwa kutokana na sababu kuwa haitaweza kuweka maandalizi yafaayo ya kusahihisha mtihani huo ikitumia walimu.
Hili ni kinyume na jinsi ilivyokuwa ikitoa mitihani yake ya hapo awali ambapo ilimhitaji mwanafunzi kufikiria jibu na kuliandika moja kwa moja katika mapengo yaliyoachwa wazi.
Sasa itawabidi walimu wanaofunza Gredi ya 6 waanze kuwafundisha wanafunzi upya jinsi ya kujibu mtihani wa aina hiyo.
Ingawaje jambo hilo si gumu kulitenda, walimu wanaachwa wakijiuliza maswali yasiyo na majibu kuhusu iwapo kuna tofauti yoyote kati ya KCPE na KPSEA na kama mfumo wenyewe wa CBC umetekwa nyara.
Pana kila sababu ya kufikiria kuwa huenda elimu hii ya CBC haitakuwa na tofauti sana na ile ya 8-4-4 ikiwa mitihani itatayarishwa hivyo.
Ingawa KNEC inasema kuwa alama za mwisho za mwanafunzi zitakuwa ni jumla ya mitihani aliyofanya mwanafunzi katika Gredi ya 4, 5 na 6, kuna hofu kuwa kuna wanafunzi wengi sana wasiokuwa na alama hizo kutokana na changamoto za kuwasilisha alama hizo kwa KNEC na pia walimu wengi kukosa ufahamu wa vile walivyostahili kufanya.
Kwa upande mwingine, huenda alama zilizowasilishwa kwa KNEC na baadhi ya walimu hazikuwa za haki. Kuna wale walimu hawawajibiki ipasavyo na huenda waliwapa wanafunzi wao alama wasizostahili.
Jambo kama hili litasababisha ukosefu wa uadilifu na uaminifu katika matokeo ya mtihani huo. KNEC ilifaa kuona shida hizi mapema na kutayarisha mbinu mwafaka za kuwatathmini wanafunzi.
Kuna uwezekano mkubwa kuwa KNEC imetambua kuwa usahihishaji wa mitihani ya CBC ya Gredi ya 6 kupitia kwa walimu utakuwa na gharama ya juu sana. Ndiposa ikaamua kutumia mashine katika usahihishaji wake.
Ikiwa hii ndiyo sababu, itabidi KNEC iandae vyema njia za kutafsiri matokeo ya mtihani huo ambazo hazitahujumu talanta za wanafunzi kama zilivyokuwa zikikuzwa na walimu wakiwafunza wanafunzi wao.
Hatimaye, KNEC inafaa kuelezea walimu jinsi ambavyo matokeo ya mtihani wa Gredi ya 6, KPSEA, yatakavyoathiri maendeleo ya masomo ya wanafunzi hawa katika Gredi ya 7 ambayo ni Sekondari.Kufikia sasa, hakuna aliye na mwao jinsi watoto hao watakavyojiunga na sekondari.