[ad_1]
IEBC yasitisha usajili wa wapigakura wapya kuanzia Mei 4, 2022 hadi Machi 13, 2023
NA CHARLES WASONGA
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itasimamisha shughuli ya usajili wa wapigakura wapya katika afisi zake za maeneo bunge, kaunti na katika makao makuu jumba la Anniversary Towers, Nairobi, kwa mwaka mmoja kuanzia Mei 4, 2022.
Kwenye toleo maalam la gazeti rasmi la serikali la Aprili 28, tume hiyo pia imesitisha shughuli ya kubadilisha kwa vituo vya kupigia kura kwa muda wa miezi tisa.
Shughuli hizo mbili zitarelewa mnamo Machi 13, 2023, kulingana na ilani hiyo iliyotiwa saini na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati.
“Hatua hiyo imechukuliwa ili kutoa nafasi kwa utayarishaji wa sajili kamili ya wapigakura ili kutoa nafasi kwa wapigakura kuikagua kuhakikisha kuwa maelezo yao yote ni sahihi,” Bw Chebukati akasema.
Shughuli za usajili wa wapigakura wapya na kubadilishwa kwa vituo vya kupigia kura pia zitasitishwa katika mataifa ya ng’ambo ambako Wakenya wanaishi na kufanya kazi.
Wakati huo huo, Bw Chebukati ametangaza kuwa shughuli ya ukaguzi wa sajili ya wapigakura itaanza mnamo Mei 4, 2022 kwa kipindi cha siku 30 hadi Juni 2, 2022.
Tume hiyo imewataka Wakenya kuhakikisha kuwa wamethibitisha maelezo yao ili wasije wakazuiwa kupiga kura Agosti 9, 2022 kwa misingi ya dosari katika maelezo yao.
“Tembelea kituo cha usajili au afisi za IEBC katika eneobunge ukiwa na kitambulisho chako au paspoti uliyotumia kujiandikisha kuwa mpigakura. Utasaidiwa kuthibitisha,” ilani hiyo ikasema.
[ad_2]
Source link