SURAYA DADOO: Israeli iwekewe vikwazo sawa na Urusi
NA SURAYA DADOO
RAIA wa Palestina waliadhimisha miaka 74 tangu kuharibiwa kwa nchi hiyo na kuimarisha taifa la Israeli.
Uharibifu huo unaofahamika kama ‘Nakba’ ulitekelezwa mnamo 1948 ambapo takribani Wapalestina 750 000 walifurushwa na vijiji na miji 500 kuharibiwa. Takribani Wapalestina 15,000 waliuawa.
Lakini inaonekana Nakba ingali inaendelea miongo saba baadaye.
Mauaji ya mwanahabari wa shirika la habari la Al Jazeera, Shireen Abu Akleh – Mpalestina aliyepigwa risasi na wanajeshi wa Israeli -ni ithibati tosha kwamba Nakba dhidi Wapalestina inaendelea.
Abu Akleh aliuawa na wanajeshi wa Israeli alipokuwa akifuatilia matukio katika eneo la West Bank. Ripoti ya uchunguzi ya serikali ya Palestina inaonyesha kuwa mwanahabari huyo aliuawa na wanajeshi kimakusudi. Hata hivyo, serikali ya Israeli ilikataa ripoti hiyo.
Mara baada ya mwanahabari huyo kuuawa Mei 11, mwaka huu, Israeli ilidai kuwa alipigwa risasi na wanajeshi wa Palestina.
Msemaji wa jeshi la Israeli hata alidai kuwa Abu Akleh alikuwa mwenye makossa kwa kufanya kazi yake. Kochav alisema kuwa Abu Akleh alikuwa ‘amejihami kwa kamera’ na alikuwa katikati ya wanajeshi wa Palestina.
Israeli ilitoa video ya kudhibitisha madai hayo lakini baadaye ilibainika kuwa ilikuwa feki.
Mashahidi, wakiwemo wanahabari walioshuhudia mauaji hayo ya kinyama, walithibitisha kuwa Abu Akleh aliuawa na wanajeshi wa Israeli.
Wakati wa Nakba mnamo 1948, Israeli ilidai kuwa maelfu ya Wapalestina waliotoroka makazi yao, waliuza ardhi yao kwa hiari kwa sababu viongozi wa Kiarabu waliwahimiza kufanya hivyo.
Kwa miaka 74, Wapalestina wamekuwa wakihangaishwa na Waisraeli.
Mamia ya Wapalestina wameuawa katika Ukanda wa Gaza.
Israeli ilipewa masharti matatu kabla ya kuidhinishwa kujiunga na Umoja wa Mataifa (UN) mnamo Mei 11, 1949; hadhi ya jiji la Jerusalem haikufaa kubadilishwa, Wapalestina waliohamishwa 1948 warejelee makazi yao na Israeli ilifaa kuheshimu mpaka uliowekwa na UN mnamo 1947.
Israeli imekuwa ikijikokota kutekeleza masharti hayo. Jamii ya kimataifa pia imesalia kimya badala ya kusukuma Israeli kutekeleza masharti hayo.
Jambo la kushangaza ni kwamba jamii ya kimataifa imechukua hatua za haraka kuadhibu Urusi kufuatia hatua yake ya kuvamia Ukraine tangu Februari, 2022.
Ni kinaya kwamba mataifa ambayo yamefumbia macho hatua ya Israeli kuvamia Palestina mara kwa mara, sasa wako katika mstari wa mbele kushutumu na kuwekea vikwazo Urusi.
Wapalestina wanapoona raia wa Ukraine wakivuka mpaka kwenda kutafuta hifadhi Poland, Hungary na Moldova, wanakumbuka jinsi walihepa na kutorokea Jordan, Lebanon na Syria wakati wa Nakba.
Propaganda inayotumiwa na Urusi ili kupata sababu ya kushambulia kwa mabomu Ukraine ndiyo inatumiwa na Israeli kuendelea kuhangaisha Wapalestina katika ukanda wa Gaza.
Tangu 2005, Wapalestina wamekuwa wakililia jamii ya kimataifa kuwekea Israeli vikwazo vya kiuchumi, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.
Waisraeli wametwaa maeneo ya West Bank. Jerusalem Mashariki, Ukanda wa Gaza na Golan kwa miaka 55 sasa.
Urusi na Israeli wamefurusha raia wa Ukraine na Wapalestina mtawalia katika maeneo wanayodhibiti – hatua inayokiuka Mkataba wa Geneva.
Kampuni kubwa za kimataifa zimekatiza ushirika wa kibiashara na Urusi kwa kuvamia lakini zingali zinashirikiana na Israeli! Kwa miaka 74, jamii ya kimataifa imekuwa ikiitaka Israeli kujichunguza yenyewe na kisha kujirekebisha. Lakini haijachukua hatua yoyote.
Jamii ya kimataifa haina budi kuikemea Israeli na kuiwekea vikwazo vya kiuchumi kwa kuhangaisha Wapalestina.
Suraya Dadoo ni mwandishi wa nchini Afrika Kusini
Twitter: @Suraya_Dadoo