KAULI YA MATUNDURA: Je, ni kwa nini Kiswahili kinafundishwa katika vyuo vikuu vingi ughaibuni?
NA BITUGI MATUNDURA
MSURURU wa makala haya ulichochewa na ushindi aliopata mwandishi, mwalimu na mhariri, Bw Ali Attas nchini Japan hivi majuzi.
Bw Attas alitambuliwa na nchi ya Japan kwa mchango wake aali kwa kuwa balozi mwema wa utamaduni wa Kenya katika muda wake mrefu wa ufundishaji wa Kiswahili nchini humo.
Tunu ya Bw Attas, aliyopewa na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Japan, Bw Tosimitshu Motegi katika Ubalozi wa Kenya, Japan ilikuwa imeandikwa kwa Kijapani.
Hilo lilininipa msukumo wa kutafakari mambo matatu. Kwanza, nilihisi ni ‘kinaya kikubwa’ mwalimu anayefundisha Kiswahili nchini Japan kutunukiwa tuzo iliyoandikwa kwa Kijapani badala ya Kiswahili.
Pili, Japan ni mojawapo ya nchi zenye vyuo vikuu ulimwenguni vinavyofundisha Kiswahili.
Vyuo hivyo ni pamoja na Osaka na Tokyo University of Foreign Studies.
Tatu, ni kwa nini Kiswahili kinachangamkiwa ulimwenguni?
Hatua ya kumtuza mwalimu wa Kiswahili nchini Japan ngao iliyoandikwa kwa Kijapani badala ya lugha anayoifunza bila shaka inaibua fahiwa kwamba, Kijapani na Kiswahili ni lugha ambazo hazina hadhi sawa.
Fahiwa hii iliibua mawazo ya lugha, utamaduni na ubepari (imperialism) katika fikra zangu. Ubepari ni hali ya uchumi unaowezesha watu wachache kuwa na mali nyingi na kumiliki uchumi wa nchi. Kundi fulani tawala linaweza kutumia lugha kudhibiti watu wengine na hivyo basi kusababisha ubepari wa kiutamaduni na lugha.
Ni kwa nini nchi kama vile Uchina, Japan, Marekani, Uingereza zinawekeza kimaksudi katika taasisi zao za mafunzo ili watu wao wajifundishe Kiswahili? Je, ni kwa sababu Kiswahili kinapendwa?
[Makala yataendelea]