Connect with us

General News

Jela maisha kwa kusaidia Al-Shabaab – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Jela maisha kwa kusaidia Al-Shabaab – Taifa Leo

Jela maisha kwa kusaidia Al-Shabaab

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA dereva wa Kaunti ya Mandera jana Jumatano alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa kitendo cha kushiriki ugaidi na kusababisha mauaji ya afisa wa polisi, alipowasaidia wapiganaji wa Al-Shabaab kuteka nyara madaktari wawili wa Cuba miaka mitatu iliyopita.

Issack Ibrein Robow, 42, pia alipewa adhabu nyingine mbili; za kifungo cha miaka 25 kwa kosa la utekaji nyara wa madaktari hao, na miaka 25 kwa kuwapeleka mateka hao hadi kwa magaidi.

Vifungo hivyo viwili vya miaka 25 vitatumika kwa wakati mmoja.Robow alisukumiwa kifungo hicho na Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Milimani Nairobi, Bi Martha Nanzushi.

Akimhukumu, Bi Nanzushi alisema kitendo hicho cha Robow, ambaye alikuwa dereva wa Dkt Assel Herrera Correa na Dkt Landy Rodriguez Hernande, kilitishia kuzorotesha uhusiano wa Kenya na Cuba, ambayo ilikuwa imefadhili madaktari kutoa huduma za afya nchini Kenya.

Baada ya kuzuiliwa mahala pasipojulikana kwa takriban mwaka mmoja, madaktari hao wawili waliachiliwa 2020 na kurudi kwao Cuba.

“Madaktari hao wataishi na woga na kovu la kutekwa nyara maisha yao yote na magaidi wa Al-Shabaab. Robow alifanya uhalifu mkubwa unaofaa aadibiwe vikali,” akasema Hakimu Nanzushi.

Wakati wa tukio hilo la utekaji nyara mjini Mandera mnamo Aprili 2019, Konstebo Mutundo Katambo aliuawa kinyama.

Robow alikuwa akiendesha gari la serikali nambari ya usajili GKA 221U Toyota Hilux.

Mahakama ilisema Katambo alipoaga mkewe alikuwa mja mzito na “sasa mwanawe yuko na umri wa miaka mitatu. Mtoto huyo hatawahi kupata malezi ya baba mzazi kutokana na ukora wa Robow.”

Vilevile, hakimu alisema dereva huyo alikosea nchi yake heshima kwa kuwasaidia magaidi kutekeleza uhalifu ambao unakemewa kote ulimwenguni.

“Afisa mwenzake Ramadhan Hassan aliyeponea shambulizi hilo, alisema anaishi kwa uchungu mwingi kufuatia mambo aliyoshuhudia na kupitia. Kitendo hicho cha ugaidi kimefanya hospitali ya Kaunti ya Mandera kutopelekewa madaktari hadi kufikia sasa. Wananchi wameumia kwa sababu ya unyama huo. (Isitoshe) magaidi hao walifanya uhusiano wa Kenya na Cuba kudorora,” alikariri Bi Nanzushi.

Hakimu Nanzushi alisema “korti inachukizwa na ugaidi na haitasita kuadhibu vikali wanaohusika.”

Aliongeza: “Kwa kosa la kwanza la kuwasaidia magaidi wa Al-Shabaab kuteka nyara madaktari hao raia wa Cuba, utatumikia kifungo cha maisha.”

Wakati huo huo, korti pia ilimwadhibu Robow kutumikia kifungo cha miezi sita kwa kujipatia kitambulisho cha Kenya kwa njia iliyo kinyume cha sheria mnamo Julai 6, 2000.

Wakili Chacha Mwita akimtetea mshtakiwa aliomba apewe kifungo cha nje, akisema ni baba wa watoto 11 wanaomtegemea.