Jinsi kampuni inavyoepushia wafugaji eneo kame kukadiria hasara
NA SAMMY WAWERU
KULINGANA na ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo, FAO – UN, Kenya ni miongoni mwa nchi tatu katika Upembe wa Afrika zilizolemewa na makali ya kiangazi.
Kaunti 23 zinaendelea kuhangaishwa na baa la ukame na njaa, athari zilizochangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi.
Zikitegemea ufugaji kujiendeleza kimaisha, wakazi wengi wanakadiria hasara kufuatia mifugo wao kufa njaa.
Maeneo hayo yanategemewa pakubwa katika uzalishaji wa nyama nchini, na tayari bidhaa hiyo inaendelea kuwa ghali, hususan mijini.
Ikiwa na makao yake makuu Rumuruti, Kaunti ya Laikipia, Ngare Narok Meat Industries Ltd imejituma kuokoa wafugaji kupitia ununuzi wa mifugo na kuichinja.
Kampuni hiyo ya huduma za nyama ilianzishwa 2007 na Rhoda Mbogo, msimamizi kundi la wafanyakazi anasema pia hutoa huduma za uchinjaji kwa wafugaji.
“Mbali na kununua mifugo, hutoa huduma za uchinjaji kwa wafugaji,” aelezea afisa huyo, akisema hutoza ada.
Hufanya uchunguzi wa kina kuhusu uhalali, uhalisia na umiliki wa mifugo.
Laikipia ikiwa mojawapo ya kaunti zilizoorodheshwa kukumbwa na ukame, hatua ya kampuni hiyo kutoa huduma za uchinjaji ni afueni kwa wakazi wa maeneo yaliyolemewa.
Ngare Narok ina soko la bidhaa zake Nairobi na Kiambu, ambapo hupakia vipande vya viungo tofauti. Ina matawi kadha katika kaunti hizo.
Isitoshe, huongeza thamani kwa kuunda bidhaa zitokanazo na nyama.
“Husambazia hoteli, mikahawa, wapishi tamba na baadhi ya maboma,” Rhoda asema.
Kampuni hiyo aidha ina kichinjio cha kisasa, chenye mashine na mitambo iliyoboreshwa kutekeleza uchinjaji na kuhifadhi nyama.
“Tuna lori na matrela ya uchukuzi yenye majokofu,” afichua Edel Oyalo, afisa.
Mifugo inapowasilishwa kituoni, hupumzika kati ya saa 24 – 48 na kupewa malisho na maji.
Hufanyiwa ukaguzi wa kina kiafya na mavetinari wa Ngare Narok, kuhakikisha nyama zinazofikia mteja ni salama.
Shughuli za uchinjaji hufanywa kwa kutumia nguvu za umeme, mfumo unaoepushia mifugo uchungu kupita kiasi.
Dkt Victor Yamo kutoka shirika la kutetea haki za wanyama duniani, ndilo World Animal Protection, anasema mifugo wanapohisi uchungu mwingi huachilia homoni ambazo huathiri nyama.
“Ubora wa nyama huishia kuwa duni, kama vile kuwa ngumu,” atahadharisha afisa huyo ambaye ni meneja wa kampeni za haki za wanyama.
Rhoda anaiambia Akilimali kwamba Ngare Narok huhakikisha damu imetoka ipasavyo, nyama zinaning’inizwa kwa muda hivyo basi kuwa laini na mwororo.
“Damu inaposalia kwenye nyama huchangia kuwepo kwa pathojeni na vijidudu kuibuka.”
Baadaye, hupakia kwenye mifuko kiasi kuwa hakuna mwanya wa hewa kuingia.
Kando na majokofu, pia huhifadhi kwenye vyumba vya barafu.
Ngare Narok ilikuwa miongoni mwa washirika katika sekta ya ufugaji waliohudhuria Nairobi KICC Meat Expo, mwishoni mwa mwaka 2021 kuonyesha mifumo na teknolojia za kisasa waliyokumbatia.
Kenya Meat Commission (KMC), ni taasisi ya serikali inayoangazia masuala ya nyama nchini.
Septemba 2020, Rais Uhuru Kenyatta alifanya mageuzi katika shirika hilo mabadiliko yanayotarajiwa kuleta afueni katika sekta ya ufugaji hasa kuokoa mifugo inayofariki wakati wa ukame.