Jinsi mitihani ya CBC kwa Gredi 6 itakavyotolewa
NA FAITH NYAMAI
WANAFUNZI wa Gredi 6 watafanya mitihani ya kuchagua jibu sahihi kati ya majibu mengi, katika awamu ya mwisho ya Mtihani wa Kitaifa wa Elimu ya Msingi (KPSEA).
Mkurugenzi wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchini (KNEC), Dkt David Njengere, Ijumaa alituliza hofu ya watahiniwa na wazazi kwamba mtindo wa mitihani hiyo umebadilishwa, kutoka muundo asilia wa Mtaala Mpya wa Elimu (CBC).
“Mitihani tayari imeandaliwa na ipo tayari. Hakuna kilichobadilika kwa sababu huu ndio mtihani wa kwanza kuwahi kufanyika chini ya CBC,” alisema Dkt Njengere.
Mkurugenzi huyo wa Knec alifafanua kuwa KPSEA hufuata maelekezo ya Mfumo wa Mtaala kuhusu Elimu ya Msingi, yaliyotolewa na Wizara ya Elimu mnamo 2019 kuelekeza mitihani ya kitaifa.Mfumo huo ulibuniwa na Taasisi ya Ustawi wa Mitaala Nchini (KICD).
Alisema mitihani ya kitaifa ya Gredi 3, 4, 5 na Gredi 6 ilikuwa ya maandalizi ambapo wanafunzi watafanya ule wa mwisho watakapokamilisha Gredi 6.
“Wanafunzi wa Gredi 6 tayari wamefanya mitihani ya utendaji, na wamepangiwa kufanya wa kutamatisha gredi mwishoni mwa mwaka huu ambapo kimsingi utahusu kuchagua jibu sahihi kati ya majibu kadhaa watakayopewa,” alieleza mkurugenzi huyo.
Kulingana na ripoti ya jopokazi la CBC, majaribio shuleni yatakuwa ya utendaji.
Kwa wanafunzi wa madarasa ya chini katika shule za msingi, mitihani inahusu masuala ya kimsingi; kumaanisha kuwa wanafunzi wa kuanzia Gredi 1 hadi 3 hufanya majaribio darasani.
Knec kufikia sasa imebuni vifaa rasmi vitakavyopewa wanafunzi na walimu katika shule zao ili kujazwa alama.
Baadaye shule zitakabidhi matokeo kwa kila mwanafunzi kupitia muundo maalum wa Knec, ili kuwezesha uchanganuzi wa kiwango cha ufanisi wa CBC kitaifa.
Mitihani katika madarasa ya juu ya msingi inaambatana na sera ya Elimu ya Msingi inayosimamia vipimo kati ya utendaji na ukamilishaji.
Ripoti ya jopokazi inafafanua kuwa hii inasaidia kutathmini kikamilifu uwezo wa wanafunzi na ujuzi wao katika nyanja mbalimbali.Matokeo ya mitihani ya utendaji na ukamilishaji yatatumika katika uteuzi wa wanafunzi kujiunga na shule za sekondari tangulizi – junior secondary – Januari 2023.
“Mtindo wa majaribio utakuwa mchanganyiko wa mitihani ya utendaji inayotolewa na mwalimu katika Gredi 4, 5 na 6 kisha mtihani wa ukamilishaji utakaotolewa na Knec mwishoni mwa Gredi 6,” ilisema ripoti.
Dkt Njengere alisema mitihani ya utendaji itakayofanywa katika Gredi 4, 5, na 6 itachangia asilimia 60 ya alama za jumla za wanafunzi katika gredi ya mwisho.
Nayo mitihani ya ukamilishaji ambayo imepangiwa kufanyika Novemba itachangia asilimia 40 ya alama hizo.
“Mtihani wa ukamilishaji utawapa wanafunzi wote nchini fursa ya kujiunga na shule zenye miundomsingi ya juu na utamaduni wa matokeo bora,” ilisema ripoti ya jopokazi.
Next article
Sampuli za wanaohofiwa kuugua ‘monkeypox’ kupimwa…