Jopo kuamua hatima ya jaji Chitembwe
NA JUMA NAMLOLA
JAJI Said Juma Chitembwe atasubiri ripoti ya uchunguzi wa Jopo Maalumu ili kujua kama atarejeshwa kazini au la.
Kwenye ilani iliyochapishwa Katika Gazeti rasmi la Serikali Jumanne, Rais Uhuru Kenyatta alimsimamisha kazi jaji Chitembwe hadi uchunguzi kuhusu ufisadi na utumizi mbaya wa mamlaka ukamilike.
“Baada ya kupokea ombi la Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) na kwa kutekeleza mamlaka niliyopewa na Kifungu cha 168 (5) (b) cha Katiba, ninaamuru kwamba jaji Said Juma Chitembwe, Jaji wa Mahakama Kuu ya Kenya, anasimamishwa kazi na kuondolewa ofisini mara moja,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyosambazwa kwa vyombo vya habari hapo jana Alhamisi.
Kifungu alichonukuu Rais Kenyatta kinasema, “Ndani ya siku 14 baada ya kupokea ombi rasmi, Rais atamsimamisha kazi jaji, kwa mujibu wa mapendekezo ya Tume ya Huduma za Mahakama (JSC). Na endapo jaji anayehusika si jaji Mkuu, Rais atabuni Jopo Maalum la wanachama saba.”
Jopo hilo Maalumu litaongozwa na Jaji Grace Mumbi Ngugi wa Mahakama ya Milimani, Nairobi.
Wanachama wengine ni; Majaji Abida Ali Aroni na Nzioki wa Makau. Pia kuna aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Elimu ya Uanasheria Dkt Fred N. Ojiambo, wakili James Ochieng’ Oduol, Luteni jenerali Mstaafu Jackson W. Ndung’u na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Walimu (TSC), Dkt Lydia Nzomo.
Watasaidiwa na mawakili Kiragu Kimani, Joseph Gitonga Riungu na Edward Omotii Nyang’au.
Makatibu wa jopo hilo ni Katibu katika Afisi ya Rais anayesimamia masuala ya Sheria, Bw Jasper M. Mbiuki na Katibu wa Utawala katika afisi hiyo, Bi Sarah Yamo.
Mtaalamu wa masuala ya sheria Bw Bobby Mkangi anasema Katiba kwa makusudi haikuweka muda wa Jopo Maalumu, ili kutoa nafasi kwa pande zote mbili kupata ushahidi na utetezi, lakini kwa kuzingatia haki za mtuhumiwa.
“Kutokana na uzito wa suala la kuondoa jaji ofisini, Katiba haikuweka muda wa jopo lililoundwa. Ninachojua ni kuwa yote yatategemea jinsi jaji Chitembwe atakavyoharakisha au kuchelewesha kujitetea,” akasema Bw Mkangi.
Mnamo Mei 4, 2022, JSC ilimwandikia Rais Kenyatta barua baada ya kuridhika na ushahidi uliokuwa umewasilishwa dhidi ya Jaji Chitembwe.
Ushahidi huo ulitokana na maombi kadhaa ya mawakili wa Nairobi. Kupitia Francis Wambua, walalamishi walimtuhumu Jaji Chitembwe kwa utovu wa nidhamu, uzembe, ufisadi, pamoja na kujihusisha na mambo yanayokinzana na shughuli zake kama jaji.
Aidha, JSC ilichukua ushahidi kutoka kwa aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko, baada ya kusambaza video mitandaoni zikidai Jaji Chitembwe alikuwa akiitisha hongo.
Bw Sonko alidai mbele ya JSC kuwa kutoelewana kwake na jaji Chitembwe kulihusiana na umiliki wa kipande cha ardhi katika Kaunti ya Kwale.
Jaji Chitembwe aliwasilisha pingamizi akisema video na sauti zilizorekodiwa na Bw Sonko bila idhini yake na tarehe za kurekodiwa huko, haziwezi kubainishwa.
Lakini baada ya JSC kutupa maombi yake, sasa Jaji Chitembwe atapokea mshahara nusu hadi siku Jopo Maalumu alilounda Rais Kenyatta likamilishe kazi yake.
Next article
KPA: Mbinu mpya ya ajira yapingwa kortini