Kalonzo abaki mpweke Raila, magavana wakisusia mkutano
NA PIUS MAUNDU
KIONGOZI wa Wiper, Kalonzo Musyoka jana Jumapili alibaki mpweke baada ya Kinara wa ODM, Raila Odinga na magavana wa kaunti za Ukambani kususia mkutano alioandaa katika mji wa Wote, Kaunti ya Makueni.
Bw Odinga na Magavana Alfred Mutua (Machakos), Charity Ngilu (Kitui) na Kivutha Kibwana (Makueni) walikosa kuhudhuria mkutano huo uliofaa kufanyika katika kanisa la ATG.
Askofu wa kanisa hilo, Francis Musili alisema Bw Odinga alikuwa amemhakikishia kuwa angehudhuria mkutano huo.
Waliokuwepo kwenye mkutano huo ni kiongozi huyo wa Wiper, seneta wa Makueni Mutula Kilonzo, mbunge mwakilishi wa kike, Rose Museo na aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko.
Bw Musyoka aliandaa mkutano huo na kuwaalika magavana hao kwa kile kilielezwa kuwa kurejesha heshima ambayo jamii hiyo imepoteza kisiasa.
Hata hivyo, aliwataka magavana hao wamuunge mkono akisema wameshindwa kumsaidia kuingia uongozini.
Vita hivyo vya kisiasa vimesababisha eneo hilo kupunguza kampeni za Bw Odinga tangu Bw Musyoka alipoungana na Bi Ngilu na Profesa Kibwana katika Azimio la Umoja kumuunga Bw Odinga kuingia Ikulu.
Jumapili, Bw Musyoka na viongozi wa kidini walitoa wito kwa wakazi kuungana na kudumisha amani.
Kwingineko, Profesa Kibwana alisema kuwa wanachopaswa kufanya ni kubaini kiini cha utengano baina ya viongozi wa eneo hilo.
“Tunafaa kujiuliza ajenda ya kuungana na ni serikali gani itatuunganisha. Katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, tunafaa kuwachagua viongozi walio na uwezo wa kutuunganisha wala sio vyama,” akasema Profesa Kibwana.
“Sisi magavana wa Ukambani tuliombwa tusimamishe kampeni kwa muda kwa sababu Bw Musyoka anatafuta nafasi ya kuwa naibu wa Raila. Tutasubiri kwa kuwa hatuwezi kufanya kampeni ikiwa hakuna nafasi ya kujipigia debe,” akasema Profesa Kibwana.