Kalonzo akana madai ya kutoa masharti kwa Raila
Na CHARLES WASONGA
KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amekana madai kuwa ametoa masharti makali kwa kiongozi wa ODM Raila Odinga kabla ya muungano wa One Kenya Alliance (OKA) kukubali kushirikiana na Azimio la Umoja.
Huku akijibu ripoti zilizochapishwa magazetini Jumapili, Februari 6, 2022, kwamba OKA imeshikilia kuwa inataka nafasi ya mgombea mwenza wa Odinga, Bw Musyoka alisema hajawahi kutoa masharti kama hayo.
“Leo katika magazeti, mliona waliandika kwamba OKA imetoa masharti ya kujiunga na Azimio. Mimi si mtu mwenye hulka na tabia kama hiyo. Uongozi wa serikalini hutoka kwa Mungu. Kwa hivyo, nataka kuwaambia kuwa wanakaribishwa OKA, sio OKA kujiunga na wao,” Bw Musyoka akasema.
Alisema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa kisiasa katika mtaa wa Huruma, Nairobi, Jumapili, Februari 6, 2022.
Baadhi ya viongozi kutoka Ukambani walimshtumu Bw Musyoka kufuatia ripoti kuwa alitoa masharti kabla ya kukubali kumuunga mkono Bw Odinga.
Gavana wa Makueni Prof Kivutha Kibwana alisema Musyoka hapaswi kutoa masharti kwa Bw Odinga, huku akimtaka makamu huyo wa rais wa zamani kujiunga na Azimio la Umoja bila masharti.
“Kama mwenyekiti wa Muungano wa Kiuchumi wa Mashariki ya Kusini (SEKEB), mimi pamoja na viongozi wa Ukambani tunakaribisha OKA ijiunge na Azimio,” akasema Profesa Kibwana.
Wakati wa mkutano wake wa kisiasa mtaani Huruma, Bw Musyoka alijipigia debe kama akisema yeye ndiye anafaa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.
Alitoa wito kwa muungano wa Azimio la Umoja kuungana na OKA ili kwa pamoja waweze kuikomboa nchi kutoka kwa watu aliodai kuwa nia yao ni “kuendeleza ufisadi”.