WANDERI KAMAU: Karibu Kenya, taifa la giza
Na WANDERI KAMAU
IKIWA kitoto kichanga kilichozaliwa Kenya kingeulizwa matatizo ya mwanzo kilichokumbana nayo katika siku zake za mwanzo hapa duniani, pengine jibu lake lingekuwa: “Umeme kupotea mara kwa mara.”
Naam, serikali ya Jubilee imeigeuza Kenya kuwa ‘nchi ya giza’.
Kinaya ni kuwa, serikali iyo hiyo iliahidi kuigeuza Kenya kutoka nchi ya giza na mashaka hadi kuwa ‘jamhuri ya mwanga, matumaini na mapambazuko mapya’.
Tangu zamani, giza limekuwa likihusishwa na mikosi. Katika baadhi ya jamii, giza huashiria uwepo wa shetani. Giza huwa ishara ya ajali, laana na maafa.
Mwanzoni mwa karne ya 19, Wazungu waliofika Afrika waliipa jina ‘Bara la Giza.’
Ingawa baadhi ya wanahistoria wanasema jina hilo lilitokana na uwepo wa watu Weusi, ukweli ni kuwa asili yake ni matatizo mengi yaliyoonekana kuwaandama Waafrika.
Wakati jamii nyingi zilipokuwa zikijivunia uvumbuzi katika masuala ya kisayansi, Waafrika walikuwa wakipigana wao kwa wao.
Wazungu walipokuwa wakitafuta rasilimali asilia kuendeleza viwanda katika nchi zao, Waafrika walikuwa wakizozania mifugo kama ng’ombe na mbuzi.
Cha kushangaza ni kuwa, Waafrika bado wanaendeleza ukale huo uliopitwa na wakati.
Wakati nchi za Ulaya zinaendeleza miradi muhimu kama treni za kisasa, teknolojia za kisasa na mifumo ya uchukuzi ya kisasa, nchi nyingi barani humu bado zinajikokota kuboresha mfumo wake wa kusambaza umeme.
Umeme huwa ndio msingi wa taifa lolote kuboresha uchumi wake.
Sababu ni kuwa, viwanda haviwezi kustawi bila umeme. Ni kama gari—ambapo haliwezi kusonga bila injini.
Vivyo hivyo, maswali yanayoibuka ni: Kenya itastawisha vipi uchumi wake chini ya mfumo hafifu wa kusambaza umeme kama sasa? Ni vipi tutastawisha uchumi wetu ikiwa tutaendelea kutegemea kampuni moja inayodhibitiwa na serikali kusambaza umeme?
Ukweli ni kuwa, Kampuni ya Umeme Kenya (KP) imeshindwa kutekeleza majukumu yake. Ni shirika linalofanana na gari kweche—gari kuukuu lililoharibika injini yake. Haliwezi kusonga hata kidogo.
Limeigeuza Kenya kuwa Wana wa Israeli walipotesekea jangwani kwa miaka 40 walipokuwa wakielekea nchini Kanani.
Ingawa Waisraeli walikuwa na matumaini ya kufika Kanani, Wakenya hawana matumaini yoyote.
Ahadi za serikali kuimarisha usambazaji wa stima zimegeuka kuwa maneno matamu yasiyotimizika hata kidogo.
KP imegeuka mateka wa makundi yanayoshindania udhibiti wake. Ni kama mateka aliyezungukwa na magaidi waliojihami kwa bunduki kali.
Je, chini ya mfumo dhalili kama huo, ni vipi Kenya itapata wawekezaji kutoka nje? Ni vipi tutaboresha uchumi wetu kuwa wa saa 24 kama nchi nyingine za Ulaya na Amerika? Ni vipi tutaboresha hospitali zetu bila kuhatarisha maisha ya wagonjwa wanaotegemea mitambo inayoendeshwa na stima?
Kutia msumari kwenye kidonda, bei ya stima nchini imebaki kuwa ghali kwa mamilioni ya Wakenya wanaoitumia kwa shughuli zao za kila siku. Hawawezi kumudu bei hizo!
Lawama kuu zinaelekezwa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto.
Wameifanya Kenya kuwa nchi ya mateso, dhuluma na vilio kwa yeyote anayetegemea stima kujiendeleza kimaisha.
Wakati wa vitendo ni sasa. Tumechoshwa na ahadi hewa!
[email protected]
Next article
ODM sasa yapiga UDA chenga Kilifi