Kaunti yaonya vilabu ikivitaka vipunguze kelele
NA MAUREEN ONGALA
SERIKALI ya kaunti ya Kilifi imeonya wamiliki wa maeneo ya burudani wanaocheza muziki kwa sauti ya juu bila kuwa na vibali.
Gavana wa Kilifi , Bw Amason Kingi, alisema baadhi ya vilabu katika kaunti hiyo hucheza muziki wa juu ambao husababisha usumbufu na kutatiza hali ya usalama.
Akizungumza mjini Kilifi, Gavana Kingi alisema serikali ya kaunti pamoja na ya kitaifa imeweka orodha ya maeneo ya burudani ambayo yamekuwa sugu licha ya kupewa onyo, na kusema yatapokonywa vibali vya kufanyia kazi.
“Tunapowapea leseni za kufanya biashara hiyo sio sababu ya kukosesha watu usingizi. Tukishirikiana na serikali ya kitaifa tutawafungia kufanya biashara tena katika kaunti hii,”akasema.
Gavana Kingi alisema Ijumaa wiki hii timu ya serikali ya Kaunti na ile ya serikali ya kuu watakuwa na kikako kujali njia mwafaka ya ni vipi biashara za sehemu za burudani itakavyoendeshwa.
Onyo la Gavana wa Kilifi liwania siku chache baada ya Bw Feisal Bushuti Mkongo mmoja mwenye umri wa miaka 30 kuuawa katika klabu cha Lexo mjini Kilifi.
Wakazi katika maeneo ya klabu hiyo wamekuwa wakilalamikia kelele na mziki unaochezwa kwa sauti hali ambayo iliwasukuma kuwasilisha kesi kotini.
Hapo awali wadau katika kamati ya usalama kaunti ya Kilifi wakiongozwa na kamshina wa kaunti hiyo Bw Kutswa Olaka walitaka serikali ya kaunti ya Kilifi kutufilia leseni za sehemu za burudani ambazo zimekuwa kero kwa umma kwa sababu ya muziki wa juu.
Kamati hiyo ilitaka serikali ya kaunti kukagua tena sehemu hizo na kupeana vibali upya. Kulingana na Bw Olaka alisema baadhi ya vilabu katika zinacheza mziki ya kuu kwa masaa ishirini na nne.
Alisema licha ya kuwa kelele hizo zinawakosesha wakazi usingizi,pia inawaathiri wanafunzi ambao hawawezi kusoma kwa amani wakiwa nyumbani.
Bw Olaka alisema kuwa juhudi za serikali ya kitaifa kuingilia kati kudhibiti vilabu hizo haikufua dafu kwani zinapewa vibali vya kufanya kazi na serikali ya kaunti.
“Tumepata malalamishi kutoka kwa wananchi kuhusu kelele kutoka kwa sehemu za burudani.Tulijaribu kufatilia lakini tukapata kuwa changamoto inatokea katika serikali ya kaunti ambao huwana leseni ya kuendesha biashara hizo,”akasema.
Sehemu nyingi za burudani katika kaunti ya Kilifi ziko katika maeneo wanakoishi watu na shule pia.