KIVUMBI kikali kinatazamiwa kushuhudiwa kuanzia wikendi ijayo kwenye kampeni za kufukuzia taji la Nairobi West Regional League (NWRL) muhula huu.
Timu ya Kemri FC ni kati ya vikosi vinavyopanga kushusha kazi nzito kupigania taji hilo. Kwenye mechi za ngarambe hiyo, timu hiyo imepangwa Kundi B linalojumuisha wapinzani wengine kama KSG Ogopa FC, WYSA United, Melta Kabiria, Red Carpet FC na Shalom Yassets kati ya wengine.
”Licha ya janga la corona kuvuruga shughuli za michezo tumejipanga kiume kukabili wapinzani wetu tunakolenga kuibuka kati ya nafasi ya kwanza ili kujikatia tiketi ya kufuzu kupandishwa ngazi msimu ujao,” alisema kocha wake, David Owino na kuongeza kuwa wanafahamu hakuna mteremko msimu huu.
Kocha huyo anasema wana azma ya kupanda daraja kushiriki kipute cha Ligi ya Taifa Daraja la Pili muhula ujao. Kocha huyo anadokeza kuwa kikosi chake kimefufua mchezo wacho kwenye Ligi kinyume na ilivyokuwa msimu uliyopita.
Baada ya kushiriki mechi tisa kikosi hicho kinashikilia nafasi ya nne kwa alama 16, nne mbele ya Red Carpet FC. Katika jedwali la Kundi B la michuano hiyo, KSG Ogopa inaongoza kwa kutia kapuni pointi 25, nane mbele ya WYSA United. Nao chipukizi wa Melta Kabiria wamezoa alama 16 na kufunga tatu bora baada ya kupiga patashika nane.
Timu ya Kemri inayopania kukaza kuhakikisha inabeba taji la Nairobi West Regional League (NWRL) msimu huu.
Makocha tofauti wa vikosi vya kundi hilo akiwamo Turncliff Asiebella wa WYSA United, wamenukuliwa wakisema kwamba kampeni za muhula ni moto wa kuotea mbali ambapo ni vigumu kubashiri kikosi kitakaoibuka mshindi.
Kukuza wachezaji wengi
Anasema Kemri imepania kukuza talanta za wachezaji wengi tu ndani ya miaka michache ijayo. Tangia ianzishwe inajivunia kunoa makucha ya wanasoka wengi tu waliofanikiwa kujiunga na vikosi zingine nchini. Baadhi yao wakiwamo Jacob Onyango ambaye huchezea Bidco United ya Ligi Kuu ya Betking Premier League (BKPL).
Pia wapo Kelvin Mwangi na Jackson Oketch ambao husakatia Vihiga Bullets na Black Stars mtawalia ambazo hushiriki kipute cha Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL). Anatoa wito kwa wachezaji wanaokuja wawe wakijiamini nyakati zote wanapopata nafasi kuonesha talanta zao michezoni.
Anawaambia kuwa kujituma kwao kutachangia watambulike na kubahatika kujiunga na timu zinazoshiriki ligi za juu nchini. Kocha huyo anasema anajivunia wachezaji walio kati ya tegemeo kubwa katika kikosi chake akiwamo Bravo Kalechi na Juma Walter ambao wametikisa wavu mara saba na sita mtawalia. Anakiri kuwa wanasoka hao wameonesha wazi kuwa wamepania kujikaza wakilenga kusakatia timu ya taifa miaka ijayo.