Connect with us

General News

Kiangazi kinachoendelea chanyima Kenya nafasi ya kuuza maziwa yake Oman – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kiangazi kinachoendelea chanyima Kenya nafasi ya kuuza maziwa yake Oman – Taifa Leo

NJENJE: Kiangazi kinachoendelea chanyima Kenya nafasi ya kuuza maziwa yake Oman

NA WANDERI KAMAU

KENYA imekosa nafasi ya kuuza maziwa yake nchini Oman kufuatia athari za kiangazi kinachoendelea nchini.

Oman ilikuwa ikipanga kununua maziwa kutoka Kenya ili kuongeza akiba yake kutokana na msimu wa mfungo wa Ramadhan.

Hata hivyo, hali ya kiangazi inayoendelea katika sehemu tofauti nchini imepunguza uzalishaji wa maziwa na kuongeza sana bei yake.

Oman ilikuwa ikipanga kuagiza kiwango kikubwa cha bidhaa hiyo, lakini hali ya uzalishaji nchini haikufikia hitaji lake.

Katibu wa Idara ya Ufugaji, Bw Harry Kimtai, alitaja ukosefu wa maziwa ya kutosha kama hali iliyochangia Kenya kufutilia mbali mipango ya kuyauza nchini humo.

Majuzi, kampuni ya New KCC ilianza mazungumzo na Kampuni ya Azim Milk kutoka Oman, kwenye mpango ambapo Kenya ingeongeza mapato yake ya uuzaji maziwa kwa Sh100 milioni kila mwaka.

Mpango huo ulikuwa Kenya kuiuzia Oman maziwa yasiyo na kemikali aina ya Lactose kwa muda wa miaka mitano.

“Oman ilitaka maziwa zaidi kutoka kwetu kutokana na ongezeko la uhitaji wa maziwa katika nchi yao. Hata hivyo, hatukuweza kutosheleza kiwango ilichotaka kutokana na kiangazi kinachoendelea nchini,” akasema Bw Kimtai.

Kenya imekuwa ikilenga kupanua soko lake la maziwa kwa kuuza bidhaa kama siagi katika ukanda wa Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani.

Hali ya kiangazi inayoendelea nchini imechangia bei za bidhaa hiyo kupanda kutokana na upungufu wake mkubwa.

Mnamo Januari, Kenya ilirejelea uuzaji wa mifugo nchini humo baada ya kusimamisha uuzaji wake kwa miaka 16.Mwezi huo, Kenya ilisafirisha jumla ya mifugo 40,000 yenye thamani ya Sh200 milioni nchini Oman.

Meli iliyobeba mbuzi na kondoo 14,000 kutoka sehemu tofauti nchini iliondoka katika Bandari ya Mombasa ikielekea katika Bandari ya Salalah (Oman), baada ya mataifa hayo mawili kutia saini upya mkataba wa kuboresha upya biashara ya mifugo.

Kenya ina uwezo wa kuuza zaidi ya mifugo 500,000 kila mwaka, ambapo inatarajiwa kusafirisha mifugo nchini humo na mataifa mengine katika eneo la Ghuba kila mwezi.